Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 24/02/2024

2024 FEBRUARI 24 JUMAMOSI: JUMA LA 1 LA KWARESIMA
Mt. FlavianĀ 
Kumbukumbu
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Kum 26:16-19

Musa aliwaambia watu: Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote.  Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote; na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, kama alivyosema.

Wimbo wa Katikati. Zab 119:1-2, 4-5, 7-8

1. Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote. (K)

(K) Heri walio kamili njia zao,
       Waendao katika sheria ya Bwana.
  

2. Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti
Nizitii amri zako. (K)

3. Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.
Nitazitii amri zako,
Usiniache kabisa. (K)

Injili. Mt 5: 43-48

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

TAFAKARI

TUSIBAGUANE KWANI SOTE TU SAWA MBELE ZA MUNGU: Upendo hauna mipaka, haubagui, upendo hauna dini wala kabila mbele ya Mungu. Kama vile Mungu alivyo chanzo na asili ya upendo, naye hatubagui sisi viumbe wake, ndivyo inavyotupasa nasi kutobaguana. Huu ndio wito wa Kristo kwetu. Dhana hii ya kupendana bila ubaguzi inahimizwa na Yesu kwa namna ya pekee katika maelezo aliyowapatia wanafunzi wake. Yesu anawasihi kuwa jambo waliloambiwa ya kuwa wawapende jirani zao na wawachukie adui zao, si sawa. Yesu anaweka upendo kwa wote kwa kuhimiza kuwa wawapende adui zao pia, kwani Mungu aliyetuumba wote, hutoa baraka kwa wote bila ubaguzi. Haya yote ndio tunayoimarishwa na Musa kuwa Bwana Mungu atuamuru kuzishika Amri na hukumu zake. Tumemwungama Bwana kuwa ndiye Mungu na ya kwamba tutafuata maongozi yake. Wapendwa, maisha yetu bila taratibu hayafai na hayaendi, utaratibu tuliopewa na Mungu ni kwamba watu wote tupendane. Katika kupendana tunajaliana, tunamwungama Mungu na tunazishika Amri zake.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu, utujalie kuwapenda wote bila ya ubaguzi wowote. Amina.