Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 23/02/2023
2024 FEBRUARI 23 IJUMAA: JUMA LA 1 LA KWARESIMA
Mt. Polikarp, Askofu na Shahidi
Urujuani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. Eze 18: 21-28
Bwana asema hivi: mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa. Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata moja wapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana Mungu; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi? Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuicha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, na katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. Lakini ninyi mwasema,’ Njia ya Bwana si sawa.’ Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Israeli; je, Njia zangu sizo zilizo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, atakufa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.
Wimbo wa Katikati. Zab 130
1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia. Bwana, uisikie sauti yangu. Masikio yako na yasikilize Sauti ya dua zangu. (K) (K) Bwana kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? 2. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe. (K) 3. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja Na neno lake nimelitumainia. Nafsi yangu inamngoja Bwana, Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi, Naam, walinzi waingojavyo asubuhi. (K) |
Injili. Mt 5: 20-26
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia: Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho!
TAFAKARI
TUJIPATANISHE NA MUNGU, WAKATI NDIO HUU: Katika ubinadamu wetu, mawazo, maneno na matendo yetu yanaathiriwa na dhambi zetu na inatutenga na Mungu. Kwa njia ya toba tunaghairi dhambi zetu na kumrudia Mungu. Nabii Ezekieli anatueleza juu ya furaha ya Bwana kwa mwovu ambaye ameghairi maovu yake na kumrudia Bwana. Huyu hakika ataishi. Na kwa yule ambaye anaendelea katika uovu wake, ama kwa yule aliyekuwa mtu wa haki na akaacha kutenda mema akatenda maovu atakufa. Huyu ni chukizo kwa Bwana. Yesu anawaonya wafuasi wake ya kwamba haki yao izidi ile ya Waandishi na Mafarisayo ili waupate ufalme wa mbinguni, pia anawaasa juu ya matamanio na makusudio ya kufanya dhambi. Wapendwa, mastahili yetu ya kufika mbinguni yapo ndani ya uwezo na maamuzi yetu ya kufanya mabadiliko. Tunapojikuta wadhambi tujipatanishe na Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho ili tuwe wana wake wapendwa na warithi wa ufalme wa Mungu.
SALA: Ee Mwenyezi Mungu neema ya kuacha njia zetu mbovu na kukurudia Wewe. Amina.