Select Page

Itukuzwe Damu ya Yesu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 22/02/2024

2024 FEBRUARI 22 ALHAMISI: JUMA LA 1 LA KWARESIMA
UKULU WA PETRO, MTUME
Urujuani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. 1 Pet 5:1-4 

Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiyari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.

Wimbo wa Katikati. Zab 23

1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)

(K) Bwana ndiye Mchugaji wangu, sitapungukiwa na kitu. 

2. Hunihuisha nafsi yangu, na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)

4. Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

Injili. Mt 16:13-19

Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.  Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

TAFAKARI

WEWE NDIWE PETRO: Mama Kanisa anatualika kuadhimisha Sikukuu ya Ukulu wa Mt. Petro. Ni Sikukuu inayoadhimisha mamlaka ya Mt. Petro ya kuongoza kondoo wa Bwana Yesu aliokabidhiwa. Ni Sikukuu ya kuadhimisha Kiti-Cathedrali kama alama ya uwezo wa kutawala na kuwaongoza waumini. Ni Sikukuu inayoadhimisha uwajibikaji na utunzaji wa kondoo wa Bwana Yesu aliokabidhiwa Mt. Petro. Ni Sikukuu inayoadhimisha alama ya umoja wa Wakristo inayoonekana kupitia kiti cha Halifa wa Kristo, yaani Mt. Petro. Pia Sikukuu hii hutukumbusha kuwa Mt. Petro na mahalifa wake, yaani Maaskofu wa Kanisa Katoliki, wamewekwa Mawakili wa Yesu hapa duniani. Kazi yao ndio kuyalinda salama na kuyaeneza mafundisho ya Kristo jinsi yeye alivyoliagiza Kanisa lake. Tunapoadhimisha Sikukuu ya Ukulu wa Mt. Petro, tunaalikwa kumwombea Baba Mtakatifu, Halifa wa Mt. Petro ili Mwenyezi Mungu aendelee kumwangazia Roho Mtakatifu aweze kuliongoza Kanisa la Kristo kwa neema na uchaji uliojaa upole, upendo na unyenyekevu. 

SALA: Ee Mungu Mwenyezi umlinde, umkinge na umwongoze Baba Mtakatifu siku zote.