Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/03/2024

2024 MACHI 29 : IJUMAA KUU
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Isa 52:13-53 : 12

Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu. Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo. Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu. Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa. Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatoa manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wagu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Alimhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mikononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa. Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, na kuwaombea wakosaji.

Wimbo wa Katikati. Zab 31:2-6, 12-13a, 15-16,17, 25

“1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye,
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

 

 

(K) Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

2. Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,
Naam, hasa kwa jirani zangu;
Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;
Walioniona njiani walinikimbia. (K)

3. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;
Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote. (K)

4. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

5. Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Iweni hodari, mpige moyo konde,
Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. (K)”

Somo2. Ebr 4:14-16; 5 : 7-9

Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

Yn 18:1-19 : 42 (Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo)

” M = Msomaji
W = maneno ya Watu mbali mbali
+ = maneno ya Yesu

M. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu yalivyoandikwa na Yohane.

Yesu anakamatwa.
M. Wakati ule Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni; palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawambia,
+ Ni nani mnayemtafuta?
M. Wao wakamjibu,
W. Ni Yesu Mnazareti.
M. Yesu akawaambia,
+ Ni mimi.
M. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena,
+ Mnamtafuta nani?
M. Wakasema,
W. Yesu Mnazareti.
M. Yesu akajibu,
+ Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.
M. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro,
+ Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?
Yesu mbele ya Anasi na Kayafa, Petro anamkana Yesu.
M. Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na, mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro,
W. Wewe nawe, je! hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu?
M. Naye akasema,
W. Si mimi.
M. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto, Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu,
+ Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; siku zote nalifundisha katika
sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.
M. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema,
W. Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?
M. Yesu akamjibu,
+ Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?
M. Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia,
W. Wewe nawe, je! hu mwanafunzi wake mmojawapo?
M. Naye akakana, akasema,
W. Si mimi.
M. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa
sikio na Petro; akasema,
W. Je! mimi simekuona wewe bustanini pamoja naye?
M. Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.

Yesu mbele ya Pilato.
M. Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri; lakini wao hawakuingia ndani ya ile Praitorio, wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka. Basi Pilato akawatokea nje, akasema,
W. Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?
M. Wakajibu wakamwambia,
W. Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.
M. Basi Pilato akawaambia,
W. Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!
M. Wayahudi wakamwambia,
W. Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.
M. Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa. Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia,
W. Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?
M. Yesu akamjibu,
+ Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?
M. Pilato akajibu,
W. Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta
Kwangu. Umefanya nini?
M. Yesu akajibu,
+ Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.
M. Basi Pilato akamwambia,
W. Wewe u mfalme basi?
M. Yesu akajibu,
+. Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.
M. Pilato akamwambia,
W. Kweli ni nini?
M. Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia,
W. Mimi sioni hatia yoyote kwake. Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?
M. Basi wakapiga kelele tena kusema,
W. Si huyu, bali Baraba.
M. Naye yule Baraba alikuwa mnyang’anyi. Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakamsokotea taji la miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema,
W. Salamu! Mfalme wa Wayahudi!
M. Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia,
W. Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake.
M. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia,
W. Tazama, mtu huyu!
M. Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,
W. Msulibishe! Msulibishe!
M. Pilato akawaambia,
W. Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.
M. Wayahudi wakamjibu,
W. Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.
M. Basi Pilato aliposikia neno hilo akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia, Yesu,
W. Wewe umetokapi?
M. Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia,
W. Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha?
M. Yesu akamjibu,
+ . Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu, kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.

Yesu anahukumiwa kufa.

M. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele
wakisema,
W. Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.
M. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka. Yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi,
W. Tazama, Mfalme wenu!
M. Basi wale wakapiga kelele,
W. Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!
M. Pilato akawaambia,
W. Je! nimsulibishe mfalme wenu!
M. Wakuu wa makuhani wakamjibu,
W. Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.
M. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

Yesu anasulibiwa.

M. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato,
W. Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
M. Pilato akajibu,
W. Niliyoandika nimeyaandika.

Askari wanagawanya mavazi ya Yesu.

M. Nao askari walipomsulibisha Yesu waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana,
W. Tusipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani.
M. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.

 

Yesu na mamaye.
M. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,
+ Mama, tazama, mwanao.
M. Kisha akamwambia yule mwanafunzi,
+ Tazama, mama yako.
M. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.

Yesu anakufa

M. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema,
+. Naona kiu.
M. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema,
+. Imekwisha.
M. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.

Yesu anatobolewa ubavu.
M. Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie: Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: Watamtazama yeye waliyemchoma.

 

Yesu anazikwa
M. Hata baada ya hayo Yusufu na Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe `mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akaondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi, yapata ratili mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. Na pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.”

TAFAKARI

“KIFO NI UFUNGUO WA MAISHA MAPYA
Leo Mama Kanisa anatuingiza katika simanzi nzito kwa mateso na kifo cha Yesu Kristo. Kibinadamu mtu akikata pumzi tunajua hapo ndo mwisho wake. Lakini kwa Mkristo tunaamini ni mwanzo wa maisha mengine ya umilele aidha ya furaha mbinguni (kama aliishi vyema na kufa bila dhambi) au mateso kidogo toharani (kama kuna madoa ya kutakaswa kidogo) au ya mateso milele motoni (kama alikufa na dhambi ya mauti-kumkataa Mungu hadi dakika ya mwisho). Tunavaa utu mpya baada ya kifo, (rej. 1Kor 15:42-44) “…unazikwa mwili wa kawaida na unafufuliwa mwili wa kiroho.” Somo la kwanza limemzungumzia Kristo kama mtumishi mwenye busara na somo la pili likatueleza kuwa aliingia katika mbingu kama kielelezo kwetu. Injili imetuonesha wazi kuwa Yesu alidhamiria kutukomboa kupitia mateso “kikombe alichonipa baba nisikinywe?” Kristo amekufa ili nasi tupate uzima wa mpya.”

SALA: Ee Bwana utujalie tufe kifo chema.