Select Page

Masomo ya Misa Machi 24

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/03/2024

2024 MACHI 24, JUMAPILI: DOMINIKA YA MATAWI

Rangi: Urujuani
Zaburi: Tazama sala ya siku

Injili. Mk 11:1-10

Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. Na mtu akiwaambia, mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana ana haja naye, na mara atamrudisha tena hapa. Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu. Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.

Somo 1. Isa 50:4-7

Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

Wimbo wa Katikati. Zab 22:8-9; 17a-19; 20-24

“1. Wote wanionao hunicheka sana
Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
Husema: Umtegemee Bwana, na amponye;
Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. (K)

” (K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? “

2. Kwa maana mbwa wamenizunguka;
Kusanyiko la waovu wamenisonga;
Yamenizuia mikono na miguu.
Naweza kuihesabu mifupa yangu yote. (K)

3. Wanagawanya nguo zangu,
Na vazi langu wanalipigia kura.
Nawe, Bwana, usiwe mbali,
Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. (K)

4. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni
Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni. (K)”

Mungu Wangu Mbona Umeniacha

by G.A. Chavallah

Somo 2. Flp 2:6-11

Yesu mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

KISHA INASOMWA INJILI NDEFU YA MATESO YA YESU

TAFAKARI

“UAMINIFU WETU KWA MFALME WETU ANAYEELEKEA KATIKA MATESO
Dhana ya ufalme na mateso hukinzana. Hii ni kwa sababu dhana ya ufalme huashiria mamlaka, nguvu na uwezo. Mfalme anayeambatana na mateso ni ishara ya kushindwa na kikwazo kwa wafuasi wake. Dominika ya Matawi humtambulisha Kristo kwetu katika sura hizo zote mbili: kwanza humwonesha Yeye anayepokelewa kama mfalme na watu wake na pili huishia kukamatwa, kuteswa, kusulubishwa na kuuawa msalabani. Je, inatuweka katika hali gani? Nini kinapaswa kuwa mwitikio wetu? Katika imani yetu na tunapoanza rasmi sehemu muhimu kabisa ya kipindi hiki cha Kwaresima, yaani Juma Kuu, juma ambalo kwa namna ya karibu tunayaadhimisha mafumbo makuu ya imani yetu, yaani mateso na kifo cha Kristo na kutufungulia kipindi cha Pasaka, yaani wakati wa kusherehekea ushindi wa Kristo, tunaalikwa kubaki waaminifu kwa huyu mfalme wetu anaeelekea katika mateso.
Kristo anapoingia Yerusalemu anapokelewa kwa shangwe. Wayahudi wanamlaki na kumwimbia Hosana: “ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Umebarikiwa na ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.” Neno hosana linapata asili yake toka neno la lugha ya kiebrania “hosi a na” linalomaanisha tunakuomba utuokoe. Mtunga Zaburi anaimba akisema “Ee Bwana utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi” (Zab 118:25). Watu wa Yerusalemu wanampokea Kristo kwa shangwe, wanaurandanisha ujio wake na ujio wa ufalme wa Daudi, ufalme ambao hapo zamani uliwaokoa na kuwafanya Taifa lenye nguvu sana. Sasa wanamwomba Kristo kama Mfalme wao anayekuja awaokoe: awatoe katika shida zao na kwa namna ya pekee utumwa wa utawala wa dola ya kirumi.
Lakini ghafla baada ya shangwe hizi wote wanapotea na viongozi wao wa dini wanamshitaki ili auawe na kuondolewa kwao. Anaanza kusalitiwa na wale waliokuwa karibu naye. Yuda Iskariote alimgeuka, “akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kumfaa.” Petro akakosa ujasiri na kumkana na akisema: “simjui mtu huyu mnayemnena.” Wengine walimdhiaki kwa kumtemea mate, kumvika taji la miiba na kusema: “Salamu, mfalme wa Wayahudi.” Waliokutana naye katika njia yake ya mateso hawakuona ufalme wake. “Wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako ushuke msalabani.” Na hata wafuasi wake wengine walibaki wakimtazama kwa mbali. “miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalena, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo wa Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia.”
Mazingira haya ya upepo kubadilika kwa ghafla kutupatia fursa ya kutafakari vema dhima ya siku ya leo. Shangwe yetu na hamu yetu ya kumpokea Yesu inachagizwa na nini? Je, tunauelewa sawasawa ufalme wake na utume wake? Je, hatufumbwi na matamanio ya kimwili na ya nje nje yenye kushikika tu na kushindwa kubaki waaminifu katika ufuasi wetu kwa Kristo? Bila shaka watu wa Yerusalemu na pengine Uyahudi kote walishasikia habari za Kristo kwa mafundisho yake, miujiza na uponyaji wake na kuona kuwa ndiye Masiha. Ndiye mbarikiwa ajaye kuwakomboa na ndiyo maana waliimba “hosi a na.” Changamoto nyingi za kijamii, kiuchumi na kisiasa ziliwaweka katika hali ya sintofahamu na hivyo walitaka kujikwamua. Lakini mawazo yao yaliwapeleka si katika mambo ya kweli, yaani kuustawisha ufalme wa Mungu na kuufanya ufalme wake utawale kati ya jamii ya wanadamu bali walielekea katika kutafuta ukweli kadiri ya muono wa kidunia na kukuza tamaa na mawazo ya kibinadamu.
Kristo anafikia hali hii ya kugeukwa na viongozi wa dini na kuwafanya wao kushadadia maangamizi yake kwa sababu kwa sehemu kubwa alipowafunulia ukweli na kuwataka kufundisha dini ya kweli, yaani ile dini inayoukaribisha ufalme wa Mungu wao walipinga na kuona wanaingiliwa maslahi yao na kunywang’anywa nafasi zao. Hivyo kwao alikuwa kauzibe na lazima aangamizwe. Lakini ukweli ni kwamba ufalme wa Kristo ungestawi kati yao ilikuwa ni fursa kwa kupambana na changamoto zao. Ukweli ambao unatoka kwa Mungu unaratibisha vyote kadiri anavyonuia Mungu na jamii kwa hakika inabaki katika amani na uelewano. Mazingira aliyopambana nayo Kristo yanaonekana hata leo kwa namna mbalimbali; kwa wale ambao wanafurahia na kukimbilia mambo ya imani kwa ajili yao binafsi na umaarufu wao na si kuustawisha ufalme wa Mungu.
Leo tunaalikwa kumsindikiza Mfalme wetu bila kukwazika na kupita katika hali ya mateso ili kufikia ukweli wa Injili unaosimikwa na fumbo la Pasaka. Furaha tunayoipata mwanzoni mwa imani yetu iendelee kuwa hai na kuwa na ujasiri wa kupita katika vikwazo vyote huku tukiweka mbele mapenzi ya Mungu, hata kama tutauawa, yaani kama tutapoteza haiba zetu, nafsi zetu, vyeo vyetu, sifa zetu za kijamii tuendelee kuung’ang’ania ukweli hadi mwisho ufalme wa Kristo utawale. Matukio mengi ya kusita kuutetea ukweli hutufikisha katika mfadhahiko. Mara nyingi tunapoficha ukweli huwa tunafurahia kwa muda na kuona raha lakini baadaye huwa ni mahangaiko makubwa. Tumkimbilie kwa furaha mfalme anayekuja kutuokoa, kwa hakika anakuja kutuokoa. Tubaki waaminifu katika Neno lake na tunapofanikiwa kuustawisha ufalme wake kati yetu tunaipata furaha ya kweli.
Masomo mawili ya mwanzo katika ibada ya Dominika hii yatuonesha namna ambavyo Kristo alivyobaki mwaminifu kwa mwenyezi Mungu hata kukubali kupitia hali ya mateso ili mwishoni ufalme wa Mungu utawale. Yeye alibaki yu mfalme hata pale alipoonekana anateseka, anadharaulika na hata kuuawa juu ya msalaba. Hii ni kwa sababu maana halisi ya ufalme wake ilikuwa katika kuyafanya mapenzi ya Mungu yatimie. Hata kama alionekana amedhalilika lakini katika maana halisi ya ufalme wake alibaki mwaminifu. Aliyavumilia haya yote kwa ajili yetu na mwishoni “Mungu alimwadhimisha mno na akamkirimia jina lile lipitalo kila jina.”
Ni nafasi ya kila mmoja kuingalia nafasi yake: ndani ya familia, ndani ya jamii kwa ujumla na hata ndani ya Kanisa. Je, ile «Hosiana» yako inaendelea? Kama haiendelei jiulize ni nini ambacho kimekufanya kutoweza kuona tena umuhimu wa Kristo kama mafalme, Mwokozi na mteteaji wako? Furaha ya Injili tunayoipokea mara ya kwanza inapaswa kutusukuma kuuona ufalme wa Kristo daima na kuitamka «hosiana» bila kuchoka. Tuutambue ufalme wake wakati wote nasi pia tutumike kama vyombo ya kuufunua ufalme wake wakati wote hata tupitiapo katika shida na hali ya kukata tamaa. Tufanikiwapo kupitia katika hali hiyo kwa uaminifu ufalme wake utatawala milele na hiyo itakuwa auheni na fanaka kwa ubinadamu wote unaoteseka. Nasi pia tutende kwa niaba ya wenzetu na kumthibitisha Kristo mfalme katika maisha yetu ya kila siku. Ninawatakieni maadhimisho mema ya Juma kuu.”