Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/07/2024
2024 JULAI 25: ALHAMISI-JUMA LA 16 LA MWAKA
MT. YAKOBO, MTUME
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama Sala ya Siku
Somo 1. 2 Kor 4:7-15
Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu. Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. |
Wimbo wa KAtikati. Zab 126
1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni, (K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha. 2. Ndipo waliposema katika mataifa, 3. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, Kama vijito vya kusini. Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha. (K) 4. Ingawa mtu anakwenda zake akilia, |
Injili. Mt 20:20-28
Mama yao wana wa Zebedayo alimwendea Yesu pamoja na wanawe, akamsujudia,na kumwomba neno. Akamwambia,” Wataka nini?” akamwambia, “Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.” Yesu akajibu akasema, “Hamjui mnaloliomba. Je! mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakamwambia, “Twaweza.” Akawaambia, “Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.” Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema “Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” |
TAFAKARI.
TUIKARIBISHE NEEMA YA MUNGU: Tunaadhimisha sikukuu ya mtakatifu Yakobo Mkuu. Ndiye mmoja wa wana wa Zebedayo. Alikuwa tayari kuacha aliyoyazoea awali kama mvuvi na kufuatana na Kristo akajifunza kwake na baadaye akatumwa na kuendeleza kazi ya Kristo. Yakobo alijitoa kikamilifu kutetea aliyojifunza kwa Kristo na kuyafundisha hadi kufa shahidi. Ndiye wa kwanza kufa shahidi kati ya wale mitume kumi na wawili. Tunajifunza kwa Mtakatifu Yakobo mambo mengi kama Katekisimu ya Kanisa Katoliki inavyofundisha “Wabatizwa wote wanashiriki katika maisha ya kimungu katika Utatu Mtakatifu neema ya Utakaso, neema ambayo inatufanya kuwa wana wa Mungu na wa Kanisa (KKK 263).” Neema za Mungu ni nyingi kwetu, hata tunapopata shida na changamoto mbalimbali. Tuiruhusu neema ya Mungu kufanya kazi ndani mwetu. Neema hiyo ipate mahali pa kustawi na kukomaa ndani mwetu, tuwe imara tunapokutana na majaribu au changamoto zozote zile na tupate taji la ushindi kama Mtakatifu Yakobo Mtume. Sala: Mtakatifu Yakobo mtume utuombee nasi tupate kuishuhudia Imani kwa maneno na matendo yetu. |