Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/07/2024
2024 JULAI 26: IJUMAA-JUMA LA 16 LA MWAKA
Wat. Yoakim na Anna, Wazazi wa Bikira Maria
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama Sala ya Siku
SOMO 1: YbS 44:1, 10-15
Haya na tuwasifu watu wa utauwa, na baba zetu katika vizazi vyao. Lakini hawa walikuwa watu wa utauwa, wala kazi zao za haki hazisahauliki. Wema wao utawadumia wazao wao, na urithi wao una wana wa wana; wazao wao wanashikamana na agano, na watoto wao kwa ajili yao. Kumbukumbu lao litadumu milele, wala haki yao haifutiki kamwe; miili yao imezikwa katika amani, na jina lao laishi hata vizazi vyote. Mkutano wa watu wataitangaza hekima yao, na makusanyiko watazihubiri sifa zao.
Wimbo wa Katikati. Zab. 132: 11, 13-14, 17-18
Bwana amemwapia Daudi neno la kweli, Hatarudi nyuma akalihalifu, Baadhi ya wazao wa mwili wako Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.
(K) Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni, Ameitamani akae ndani yake. Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele, Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)
Hapo nitamchipushia Daudi pembe, Na taa nimemtengenezea masihi wangu. Adui zake nitawavika aibu, Bali juu yake taji yake itasitawi. (K)
Injili. Mt. 13:16-17
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
TAFAKARI
TUOMBE KUWA NA MACHO NA MASIKIO YA KIROHO: Leo tunafanya kumbukumbu ya watakatifu Yoakim na Anna, wazazi wa Bikira Maria. Ni kutokana na mapokeo na mafundisho ya Kanisa kuwa wazazi wa mama yetu Maria ni Yoakim na Anna. Umuhimu huu wa Watakatifu Yoakim na Anna unatokana na uhusiano wao na mama yetu Maria na mwanae Yesu. Hawa ni bibi na babu wa Yesu, ni kati ya wanaotengeneza familia kubwa ya Kristo na ndio hawa wanaotupatia Kristo na mama yake Maria. Wazazi hawa ni mfano wa wazazi wenye imani kwa Mungu na wenye kuishi maisha ya familia kwa upendo na uwajibikaji. Kutoka Injili Kristo anasema ‘heri macho yenu kwa kuwa yanaona na masikio yenu kwa kuwa yanasikia.’ Haitoshi tu kuwa na macho haya ya kawaida, ila tumwombe Mungu atujalie macho na masikio ya kiroho. Macho na masikio ya kiroho ndiyo yale yanayotuwezesha kuona kuwa familia yetu ni kubwa ikihusisha pia Yoakim na Anna, na masikio ya Kiroho ni yale yanayotuwezesha kusikia na kuishi mafundisho ya Kristo.
Sala: Ee Kristo, tujalie tuwe na macho na masikio ya kiimani ili maisha yetu yachorwe na upendo wako. Amina.