Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 23/07/2024

2024 JULAI 23: JUMANNE-JUMA  LA 16 LA MWAKA

Mt. Birgita, Mtawa
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma 4

Somo 1. Mik 7:14-15, 18-20

Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.

Wimbo wa Katikati. Zab 85:2-8

1. Bwana, umeiridhia nchi yako,
Umewarejeza mateka wa Yakobo.
Umeusamehe uovu watu wako,
Umezisitiri hatia zao zote.
Umeiondoa ghadhabu yako yote,
Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.

(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako.

2. Mungu wa wokovu wetu, uturudishe,
Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.
Je, utatufanyia hasira hata milele?
Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi? (K)

3. Je, hutaki kurudi na kutuhuisha,
Watu wako wakafurahie?
Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako,
Utupe wokovu wako. (K)

Injili. Mt 12:46-50

Yesu alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia,”Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe.”Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, “Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani?”Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana yeyote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.”

TAFAKARI.

MAMA NA NDUGU ZAKE KRISTO: Fikiria ukiwa na kaka au dada maarufu, bila shaka hutachoka kumshukuru Mungu kwa ajili yake. Usingechoka watu kukuuliza habari zake huyo unayempenda. Unakuwa na uhakika wa upendeleo wa kuwafikia wapendwa wako kila wakati wa maisha yako. Sehemu ya Injili ya leo, Yesu anatuambia anayeyafanya mapenzi ya Baba yake aliye Mbinguni anafurahia kuwa karibu zaidi nami kuliko ndugu wa damu moja wa kuzaliwa. Hapa Kristo anatupatia maana mpya ya wale wanaoyapokea na kuyafanya mapenzi ya Mungu. Kwa maelezo hayo Kristo hayapunguzii uzito mahusiano ya kindugu wa damu bali anayaboresha yakijumuisha kuyafanya mapenzi ya Mungu. Yeyote anayempokea Mungu kama Bwana na Mchungaji wake, atamsikiliza na kumgeukia katika hali zote za maisha. Ni muhimu kuendelea kumsikiliza na kumgeukia nyakati zote za maisha yetu. Tumsikilize kama kaka yetu, ndiye Mwana wa Mungu aliye hai na Masiha wetu. Anatufundisha mengi sana kama vile kuwa watu wa huruma, kuishi kwa upendo na kusamehe ilivyosisitizwa katika somo la kwanza.  

Sala: Ee Bwana neema yako iendelee kutuwezesha kuyatimiza mapenzi ya Mungu siku zote. Amina.