Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 07/09/2024
2024 SEPTEMBA 7: JUMAMOSI-JUMA LA 22 LA MWAKA
Mt. Hadrian
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 2
Somo 1. 1 Kor 4: 6b-15
Ndugu zangu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu, ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe. Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea wajisifia nini kana kwamba hukupokea? Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi! Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tamaa ya vitu vyote hata sasa. Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali kuwaonya kama watoto niwapendao. Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya injili. |
Wimbo wa Katikati. Zab 145: 17- 21
1. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, (K) Bwana yu karibu na wote wamwitao. 2. Atawafanyia wamchao matakwa yao, 3. Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana; |
Injili. Lk 6:1-5
Ilikuwa siku ya sabato moja Yesu alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusapukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, “Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato?” Yesu akawajibu akawaambia, “Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao.” Akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.” |
TAFAKARI
KRISTO NDIYE BWANA WA SABATO: Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” Maneno haya ya mafarisayo yaonesha jinsi watu walikuwa wamebanwa na sheria za kiyahudi ambazo hazikusaidia watu kuishi kwa upendo hata kwa waliohitaji mambo muhimu ya maisha kama chakula. Kulingana na mitazamo yao ni afadhali mtu kufa njaa kuliko kula chakula wakati usio kubalika kisheria. Katika hali hiyo ya kutojali mahitaji muhimu ya wanadamu, Yesu anawauliza mafarisayo ikiwa hawajasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? Daudi mfalme aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyohifadhiwa, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” Katika maelezo haya, Yesu anatushauri sote kuangalia sana mazingira yetu pamoja na mahitaji ya kimsingi ya maisha na afya ya binadamu wote. Kwa hiyo hata ikibidi kuvunja amri kwa sababu ya kulinda maisha ya watu. Maana yake, Mungu ana uwezo juu maisha yote ya binadamu ili kuwepo na upendo. SALA: Tuwaombee wanaotunga sheria na kuzitumia ziweze kuwasaidia watu kuishi kwa upendo zaidi. |