Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 04/09/2024

2024 SEPTEMBA 4: JUMATANO-JUMA LA 22 LA MWAKA

Mt. Rosa wa Viterbo
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. 1 Kor 3:1-9

Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa, sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, mimi ni wa Paulo; na mwingine, mimi ni wa Apollo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apollo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apollo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.

Wimbo wa Katikati. Zab 33:12-15, 20-21

1. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Toka mbinguni Bwana huchungulia,
Huwatazama wanadamu wote pia.

(K) “Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
watu aliowachagua kuwa urithi wake. “

2. Toka mahali pake aketipo
Huwaangalia wote wakaao duniani.
Yeye aiumbaye mioyo yao wote
Huzifikiri kazi zao zote. (K)

3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Maana mioyo yetu itamfurahia,
Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takaifu. (K)

Injili. Lk 4: 38-44

Yesu alitoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.

TAFAKARI

KRISTO ANATUPONYA NA KUTUUNGANISHA KWA BABA: Bwana wetu Yesu Kristuo alifika nyumbani kwa Simon, naye mama wa mke wake alikuwa mgonjwa. Kristo alipojulishwa kuhusu mgonjwa alisimama karibu naye na akaikemea homa ikamwacha. Hapo tunajifunza kwamba Mwenyezi Mungu anawahurumia watu wake kwa njia ya Kristo tena anayeonekana na kutembea hadi kufika katika familia zetu. Yesu Kristo ni huruma na upendo ya Mungu miongoni mwa watu wake wanaoteseka na kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali. Mama mkwe wa Simoni Petro baada ya kupona aliamka mara moja akaanza kuwatumikia. Nasi tunajifunza ya kwamba ikiwa Mungu ametuinua kwa njia yoyote na kutupatia afya nzuri, tusiache kumtumikia Yeye na watu wake. Kwa upande wake, Mtakatifu Paulo anatushauri kuachana na tabia za ubaguzi miongoni mwetu. Tusijigawe kwenye makundi kwa sababu ya viongozi tunaowafuata, tuungane naye Kristo anayetuonesha njia iendayo kwa Baba.