Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/09/2024

2024 SEPTEMBA 8: DOMINIKA YA 23 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 3

sOMO 1. Isa 35: 4-7a

Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji. 

WIMBO WA KATIKATI. Zab 146:7-10

1. Bwana ndiye ashikaye kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa.
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa.

(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

2. Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
Huwainua walioinama.
Bwana huwapenda wenye haki,
Huwahifadhi wageni. (K)

3. Bwana huwategemeza yatima na mjane,
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)

SOMO 2. Yak 2:1-5

Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? 

INJILI. Mk 7:31-37

Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.

TAFAKARI

NENO LA KRISTO LINAFUNGUA VIFUNGO VYOTE
Mandhari ya jangwa hayafurahishi na hivyo katika hali ya kawaida mwanadamu hujitahidi kupambana na hali ya jangwa. Mmoja anapokuwa jangwani hana uhakika wa kupata maji au chakula, kupata kivuli na pia safari ya jangwani huonekana kuwa ni ndefu na ya kuchosha. Sehemu ya jangwa iitwayo oasis ni sehemu muhimu sana na mmoja aliye jangwani aionapo hupata furaha ya ajabu. Katika sehemu hii huonekana miti iliyostawi kwa ajili ya kupumzika kivuli cha jua kali la jangwani, hupatikana maji kwa ajili ya kutuliza kiu na mazao mengine ya kutuliza njaa. Maisha ya mwanadamu wakati wa taabu, maangahiko na mateso ya ulimwengu yanaweza kurandanishwa na jangwa. Mmoja hujiona kuwa yu jangwani kiroho na kimwili. Ni nyakati ambazo humfanya mmoja kuwa na kiu, njaa na hamu ya faraja kutoka kwa watu wanaomzunguka. Hali hii ya jangwa inaweza kumfikisha mmoja katika hali ya kukata tamaa kama hatapata tegemeo kwa wale wanaomzunguka.
Neno la Mungu dominika hii linatupatia “oasisi” ya uhakika katika jangwa la kimaisha. Huyu ni Kristo ambaye anakuja kutufungua vifungo vyote na kuturejeshea furaha na matumaini. Yesu yupo katika mipaka ya miji kumi au dekapoli inayoikabili bahari ya Galilaya. Haya ni maeneo yaliyokaliwa na wapagani. Hapa analetewa bubu-kiziwi na anamponya. Tunaweza kuelewa utendaji huu wa Kristo kwanza kwa kutafakari eneo analofanya uponyaji. Ilikuwa ni nchi ya wapagani. Upagani unawakilisha kutokuwepo Mungu. Ni watu ambao wanasafiri katika ulimwengu huu bila dira. Haya ni maeneo yaliyodharaulika na kutengwa kwa kuonekana hayafai na waishio humo hawastahili na pia hawatauona wokovu.
Pili ni hali ya huyu anayeponywa. Hali ya kuwa bubu humzuia mmoja kuweza kuongea. Hawazi kuelezea hisia zake; hawezi kufikisha maombi ya mahitaji yake; hawezi kutoa ushauri. Hali ya kiziwi inamzuia kusikia mazungumzo ya namna yoyote. Huyu anadhulumiwa namna nyingi za mahusiano ya kibinadamu. Ni sawa na yeye anayekuwa gerezani na anashindwa kujifunua kikamilifu katika kustawisha urafiki na hatimaye undugu. Kifupi mtu wa namna hii ni sawa na yule aliyetengwa na jamii inayomzunguka. Hali yake hii inafafanua vizuri zaidi hali ya ujangwa katika nchi hiyo ya kipagani. Wale ambao wanaishi bila Mungu hawawezi kuzungumza iwapasavyo na pia hawasikii vema. Watu hawa wapo jangwana; wanasafiri wakitafuta kuiona “oasisi”.
Mahali hapa palipo na ukosefu wa namna hii, mahali ambapo pametengwa na ukawaida wa kibinadamu ndipo panampatia Kristo fursa ya kufanya uponyaji wake na kuufunua utume wake ambao umenuia katika kumrudishia tena mwanadamu matumaini. Hapa anatufunulia jinsi jicho la Mungu linavyowajali watu wake na wokovu wake unawalenga watu wote. Unatimia unabii wa Isaya anayesema katika somo la kwanza: “Waambieni walio na moyo wa hofu, jipeni moyo, msiogope.” Mwenyezi Mungu anatutia nguvu na matumaini kuwa jicho lake daima limeelekezwa kwa watu wake. Jipeni moyo! Inueni macho yenu na mumtazame yeye. Uwepo wake mwenyezi Mungu unawafanya bubu kusema, viziwi kusikia na vilema kurukaruka; zaidi ya hayo anabubujisha maji katika nyika na kuchipusha vijito jangwani.
Uhakika wa uwepo wa Mungu utupeleke kutafakari zaidi sababu za mwanadamu kuingia katika hali ya jangwa. Yote ni matokeo mabaya ya dhambi ambayo yanamtenga mwanadamu na mwenyezi Mungu na kwa upande mwingine mwanadamu hutengana na mwanadamu mwenzake. Matokeo yake ni mtu binafsi kujitenga na jamii na kwa upande mwingine jamii kumtenga mtu. Hapa tunaona jinsi ambavyo tunashindwa kuidhihirisha hadhi yetu tuliyowekewa na muumba wetu kama tunu tangu wakati wa uumbaji. Hadhi hii hujipambanua katika namna ya mahusiano ya mtu na mtu. Katika hali ya ukengemfu mwanadamu anafunga masikio yake au anajifanya kiziwi na kuufumba mdomo wake asiseme lolote. Kilio cha mwenzake anayehitaji msaada pembeni yake hakisikiki. Tunagalie jinsi ambavyo tunajitengenezea hali hiyo ya jangwa. Maskini analia hatumsikii; vijana wanahangaika kutafuta kazi au riziki hatuwajali. Tunajihisi tupo katika “oasisi” lakini kwa kweli sisi ndiyo tunabaki katika jangwa.
Mtume Yakobo anaipambanua zaidi hali hiyo katika tabia ya upendeleo ambayo inaua hadhi yetu ya kuwa wana wa Mungu. Tunawatenga wanadamu na kuwapendelea wale watakaolipa. Jamii yetu inayadhihirisha hayo kwa namna mbalimbali ya matokeo yake tumetengeneza matabaka kati ya walionacho na wasionacho. Mtume Yakobo anatuonya kutokuitumia hadhi yetu kinyume na Injili ya Kristo. Injili ya Kristo ilinuia katika kuwaunganisha wanadamu wote na kuwainua walio wanyonge. Ukristo unatuita katika kujishusha, kujinyenyekeza na kuwasikiliza wahitaji na kisha kuwapatia wote kadiri ya mahitaji yao. Kristo mwenyewe amekuwa bingwa wa namna hiyo ya kujishusha katika kenosis yake (rej. Flp 2:6 – 8).
Dominika ya leo tunawekewa changamoto mbele yetu. Kwanza ni kujiangalia tunalo jangwa la namna gani? Je, tunajihisi kutengwa na jamii isiyotusikiliza? Basi hapa tunaalikwa tujipe moyo na tusiwe na hofu. Tunapaswa kuelekeza imani yetu kwa Mungu na kuyaona yote katika Yeye. Tuwe na taadhari kwani mara nyingi hali kama hizi zinashawishi au kutuingiza katika hali mbaya zaidi na hata kumwasi mwenyezi Mungu. Hivyo paji la imani ni hitajiko muhimu. Imani thabiti itatusaidia kumfanya mwenyezi Mungu abaki ndani mwetu na kutupatia ufafanuzi wa hali mbalimbali. Walimwengu wasipotusikiliza yeye atatusikiliza na kutupatia mbinu muafaka ambayo haitajenga chuki au kisasi bali upendo na msamaha hata kwa wanaotuudhi.
Je, mimi ninajihisi kuwa katika ulimwengu wangu uliotimilika? Usijidanganye! Mwanadamu hawezi kuishi kama Gendaeka, yule nyani dume anayeishi peke yake porini. Tumeumbwa kwa ajili ya kuhusiana. Uhusiano wangu na wenzangu ndiyo unaonitambulisha katika jamii. Mwenyezi Mungu ananitumia mimi kwa ajili ya kuwafungua viziwi na bubu ambao wanatuzunguka kila siku. Anategemea kutoka kwangu utimilifu wa uaguzi wa Nabii Isaya. Kujifungia kwangu katika ulimwengu wangu au utoaji wangu wa huduma kwa upendeleo unazidisha hali ya jangwa ndani yangu na ndani ya wale wanaonizunguka. Kinyume chake pale ninapojifungua na kushirikisha karama nilizopewa na Mungu hakika ninakuwa chombo cha kufikisha matumaini kwa waliopondeka na kuvunjia moyo na pia kwa walio na moyo wa hofu.
Yesu alimwambia Yule mgonjwa: “Efatha” yaani funguka. Hapo anaelezea kwa ufupi sababu ya ujio wake hapa duniani. Ni kumfungua mwanadamu na kumfanya kuwa huru. Tutoke katika majangwa na nafsi zetu; tuifungue mioyo yetu. Tunapomkaribisha Yeye aliye “oasisi” ya maisha yetu kwa hakika tutarejesha matumaini katika maisha ya mwanadamu; furaha, amani, matumaini na upendo vitatawala. Mwanadamu atarudishwa katika hali njema; atarudishiwa tena ile “paradisi” aliyonyang’anywa kwa sababu ya dhambi.

SALA: Ee Bwana ufungue masikio na midomo yetu iweze kusikia na kutangaza neno.