Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/05/2024
2024 MEI 27 : JUMATATU-JUMA LA 8 LA MWAKA
Mt. Augustine wa Canterbury, Askofu
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 3
Somo 1. 1 Pet 1: 3-9
Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kriso, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufufuliwa wakati wa mwisho. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo. Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 111: 1-2, 5-6, 9-10
1. Aleluya, (K)Atalikumbuka agano lake milele. 2. Amewapa wamchao chakula; 3. Amewapelekea watu wake ukombozi. 4. Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, |
INJILI. Mk 10:17-27
Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja, Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote. Uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu. |
TAFAKARI
KUINGIA MBINGUNI KUNADAI SADAKA: Liturujia ya Neno leo hasa Injili inaendelea kutupatia Katekesi juu ya ufalme wa Mbinguni. Yesu anatufundisha kuwa ili kuingia Mbinguni ni lazima kujitoa sadaka na kuachilia yale yote yanayoweza kuwa kikwazo. Tupo katika wakati ambao baadhi ya wenye mali hutumia vibaya mali zao kwa kutoa rushwa ili kupata upendeleo katika jambo fulani, hata kuumiza haki za wengine. Uaminifu na ukweli vinauzwa na kununuliwa kwa bei fulani cha fedha. Kwa vitendo hivi Yesu anatuonya kwa nguvu kuwa fedha zinaweza kuwa kikwazo kwetu kwenda Mbinguni. Wapo baadhi ya watu miongoni mwetu wanaosahau kabisa wajibu wa kwenda Misa siku ya Dominika na siku za amri kwa sababu ya kutafuta fedha. Tuliyemsikia katika Injili alikuwa na umotomoto wa kuwa mkamilifu ila alipotakiwa kutoa mali zake kuwa sadaka amepata sikitiko na kukataa mwaliko wa Yesu kwani alikamatwa na mali zake. Tujitazame wenyewe tuone ni jambo gani linaloturudisha nyuma katika kuitikia mwaliko wa Kristo na tumwombe Yesu Neema ya kuondokana na vitu hivyo. Sala: Ee Yesu nijalie Neema ya kuyaacha malimwengu niambatane nawe daima. |