Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/06/2024

2024 JUNI 13 : ALHAMISI-JUMA LA 10 LA MWAKA

Mt. Anthoni wa Padua, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: KIjani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. 1 Fal 18:41-46

Eliya alimwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanya mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuingia Yezreeli.

Wimbo wa Katikati. Zab 65:10-13

1. Umeijilia nchi na kuisitawisha.
 umeitajirisha sana;
 mto wa Mungu umejaa maji;
 wawaruzuku watu nafaka,
maana ndiwe uitengenezae ardhi.

(K) Ee Mungu sifa za kulaiki katika Sayuni.

2. Matuta yake wayajaza maji;
wapasawazisha palipoinuka,
Wailanisha nchi kwa manyunyu;
 waibariki mimea yake. (K)

3. Umeuvika mwaka taji ya wema wako;
mapito yako yadondoza unono.
Huyadondokea malisho ya nyikani,
na vilima vyajifunga furaha. (K)

Injili. Mt 5:20-26

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.  Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.  Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

TAFAKARI

TUWE NA MTAZAMO SAHIHI WA SHERIA ZA MUNGU: Wafarisayo ambao daima walimpinga Yesu, waliwafundisha watu kuwa mtu alihesabiwa haki pale tu alipoweza kushika sheria na vipengele vyake vyote. Fundisho hili lilileta ugumu kwa watu namna ya kujikita katika sheria (rej. Rom 7:21-24). Injili ya leo inatufundisha kuwa tunapaswa kuishi kwa kadiri ya roho ya sheria na siyo kujikita katika maneno ya sheria. Ni lazima kuondoa ndani mwetu yale yote yanayoweza kusababisha kifo, hasira, kinyongo, kutaka kulipa kisasi, kuonea wengine. Yesu anatufundisha pia kuwa namna nzuri ya kumwabudu Mungu ni kuhakikisha mahusiano yetu na wenzetu ni mazuri. Kabla ya kusali tujipatanishe kwanza na ndugu zetu ndipo sala yetu inapata kibali machoni kwa Mungu. Tukijikita katika sala bila upatanisho na ndugu zetu sala yetu haitapokelewa. Tuwe watu wa kutoa na kupokea msamaha ili nasi tuweze kufaidi matunda hayo.

SALA: Ee Mungu utujalie moyo wa kutii sheria zako.