Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 14/06/2024

2024 JUNI 14 : IJUMAA-JUMA LA 10 LA MWAKA

Mt. Eliya, Nabii
Rangi: KIjani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. 1 Fal 19: 9a. 11-16

Eliya alifika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagizo yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe. Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.

Wimbo wa Katikati. Zab 27: 7-9, 13-14

1. Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia,
Unifadhili, unijibu.
Uliposema, Nitafuteni uso wangu,
Moyo wangu umekuambia.

(K) Usinifiche uso wako, Ee Bwana.

2. Usinifiche uso wako,
    Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
    Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
     Wala usiniache, ee Mungu wa wokovu wangu. (K)

3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
    Katika nchi ya walio hai.
    Umngoje Bwana, uwe hodari,
    Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)      

Injili. Mt 5:27-32

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia, kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini. 

TAFAKARI

KUISHI ROHO YA SHERIA ZA MUNGU: Katika Injili ya leo Yesu anatufundisha thamani ya utu wetu ambao kwao tumepewa taratibu za kulinda utu huo. Katika hili Yesu anatazama uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke katika ndoa kama kielelezo cha maisha ya pamoja. Sheria iliyokataa uzinzi na kukubali talaka zinapewa ufafanuzi mpya ili kulinda na kutunza utakatifu wa ndoa. Hivyo Yesu anafundisha kuwa waaminifu katika maagano ya ndoa kwa matendo na uwazi. Katika kuishi sheria za Mungu tunasema kuwa chochote kinachosababisha kutenda dhambi na kuwa mbali na Mungu tuondokane nacho. Siku hizi tupo katika ulimwengu wenye vitu vinavyoweza kusababisha dhambi. Mfano matumizi mabaya ya simu, televisheni, pesa nk. Kama vitu hivi vinatuweka mbali na Mungu basi tusivipe kipaumbele katika maisha yetu. Kung’oa jicho au kukata mguu kwa sasa kutafsiriwe kuwa kama simu, televisheni na chochote kile ambacho kinanisababisha kutenda dhambi.

SALA: Ee Yesu utujalie neema ya kushinda hisia na vishawishi vya dhambi.