Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 24/05/2024

2024 MEI 24 : IJUMAA-JUMA LA 7 LA MWAKA

Bikira Maria, Msaada wa Wakristu
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma

Somo 1. Yak 5: 9-12

Ndugu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma. Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.

Wimbo wa Katikati. Zab 103: 1-4, 8-9, 11-12

1. Ee nafsi yangu umhimidi Bwana.
Naama, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nfsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K)Bwana amejaa huruma na neema.

2. Akusamehe maovu yako yote,
Akuponye na magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)

3. Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta siku zote,
Wala hatashika hasira yake milele. (K)

4. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)

Injili. Mk 10:1-12

Yesu alifika mipakani mwa Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.

TAFAKARI

NDOA NI AGANO TAKATIFU KATI YA MUME NA MKE: Neno la Mungu leo linatufundisha jinsi uhusiano wa mume na mke unavyopaswa kuwa. Ndoa ni muungano mtakatifu ambao chimbuko lake ni Mungu mwenyewe. Muungano wa ndoa unapaswa kulindwa kwani ni agano na siyo mkataba. Ili ndoa iweze kusimama imara ni lazima kuwepo na usawa kwa pande zote mbili yaani mume na mke. Tupo katika wakati ambao tunashuhudia ndoa nyingi zikiwa na matatizo mengi, baadhi ya wanandoa kupelekana mahakamani kuomba talaka na kuvunjika kwa ndoa. Hali hii ni hatari kwa Sakramenti ya ndoa kwani hamna ndoa ya mkataba bali ni ya kudumu. Tuombee vyombo vinavyosimamia haki za wanandoa waweze kutenda haki kwa pande zote yaani kwa mume na mke lakini pia vitende haki kwa Mungu anayewaunganisha wanandoa. Tuwaombee wanandoa wenye matatizo wajue kuwa suluhisho la matatizo yao ni msamaha na upendo wa dhati.

SALA: Ee Mungu utujalie tuheshimu maagano ya ndoa.