Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/05/2024

2024 MEI 9 : ALHAMISI-JUMA LA SITA LA PASAKA

Mt. Pakomi, Abate
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 18:1-8

Siku zile, Paulo alitoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzaliwa wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila Sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani. Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.

Wimbo wa Katikati. Zab 98:1-4

1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

(K) “Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa:”

2. Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

Injili. Yn 16:16-20

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake:  Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona. Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni na tena bado kitambo kidogo nanyi  mtaniona? na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba?  Basi walisema, neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo?  Hatujui asemalo. Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?  Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 

TAFAKARI

BAADA YA DHIKI FARAJA: Katika Injili ya leo Yesu anaendelea kuwaasa Wafuasi wake anapowaaga. Kwa muda fulani furaha yao itaondoka kwa kutokumwona tena katika mwili wa nyama ila baadaye furaha yao itarudi watakapomwona tena na kuungana naye. Huzuni yao itasababishwa hasa kutokana na kifo chake hivyo watakuwa wapweke na watapata fadhaa itakayosababishwa na wapinga Kristo. Anawahakikishia kuwa huzuni yao haitadumu bali itageuzwa kuwa furaha. Wapendwa Taifa la Mungu maisha ya ufuasi ni maisha yanayodai sadaka kubwa na uvumilivu mkubwa. Injili ya leo ni ya matumini makubwa kwetu kuwa baada ya dhiki ni faraja. Hii inamaanisha kuwa tunapobaki waaminifu kwa mafundisho ya Kristo kuna maumivu tunayopata. Maumivu hayo si kitu ukilinganisha na utukufu ujao (rej. Rom 8:18). Hivyo adha ziletwazo na maisha ya ufuasi zisiturudishe nyuma kwani mwisho tutapata tuzo.
SALA: Ee Yesu utujalie furaha na faraja hata katika dhiki na huzuni zetu.