Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 15/04/2024

2024 APRILI 15 : JUMATATU-JUMA LA TATU LA PASAKA

Mt. Paterno, Askofu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 6:8-15

Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima ya huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi; wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.

Wimbo wa Katikati. Zab 119:23-24, 26-27, 29-30

“1. Wakuu nao waliketi wakaninena,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako,
Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu. (K)
2. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundishe amri zako.
Unifahamishe njia ya mahusia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako. (K)

3. Uniondolee njia ya uongo,
Unineemeshe kwa sheria yako.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. (K)”

(K) Heri walio kamili njia zao.

Injili. Yn 6:22-29

Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja; tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao. Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru. Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.

TAFAKARI

TUHUBIRI DAIMA KWA FURAHA: Mashtaka dhidi ya Stefano yanafanana sana na yale mashtaka dhidi ya Yesu. Hata katika mashtaka haya maajabu yanaonekana kwa Stefano. Wakati washtaki wake walikuwa na nyuso zilizokunjamana kwa hasira na ghadhabu, uso wa Stefano ulikuwa “kama uso wa malaika”(Mdo 6:15). Uso wake uling’aa, ukaangaza, ulitoa nuru na mwanga kwa washtaki wake. Uso wake haukuwa na hila yoyote, ukawa kama uso wa Yesu alipogeuka sura kule mlimani (rej. Mt. 17:1-13; Mk. 9:2-13; Lk. 9:28-36). Katika kuhubiri neno la Mungu, Wakristo tutegemee visa na mikasa, chuki na uadui kunakopelekea mashtaka ya uwongo dhidi yetu. Na wakati mwingine haya yatatoka kwa watu wa jamaa zetu, ndugu na marafiki. Tukikumbana na hayo Stefano anatufundisha kuyapokea kwa uso wa tabasamu uliojaa furaha, tukiendelea kung’aa mbele ya washtaki na watesi wetu ili wauone mwanga wa ukweli.

SALA: Ee Yesu ujalie furaha ya kiinjili katika ufuasi wetu.