Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 02/04/2024

2024 APRILI 2 : JUMANNE-JUMA LA KWANZA LA PASAKA

Mt. Fransisko wa Paulo, Mweremita
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Mdo 2:36-41

Petro aliwaambia Wayahudi: Nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukahidi. Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.

Wimbo wa Katikati. Zab 33:4-5,18-20, 22

“1. Neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)

Nchi imejaa fadhili za Bwana.

2. Jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)

Injili. Yn 20:11-18

Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

TAFAKARI

KUJITAMBUA KWAFAA KWA WOKOVU: Kuna mtaalamu mmoja anaitwa Euripides alisema “Marafiki wa kweli ni wale wanaokujia wakati wa taabu/shida.” Mariamu Magdalena ni kati ya marafiki waliojitokeza hadi baada ya kuzikwa kwa Yesu na alienda mahali alipozikwa Yesu. Huenda hii ilikuwa ina msukumo wa kushuhudia ufufuko lakini hakujua, au uchungu aliokuwa nao baada ya Yesu kufa haukuwa umeisha. Huyu mama alijitambua na kujitambua huko kumemsaidia kupata bahati ya kushuhudia ufufuko na kujichotea neema kwa uzima wake. Hata katika somo la kwanza baada ya Petro kuonesha ujasiri wake, umewasaidia Wayahudi kujitambua na kutaka kujua taratibu za nini cha kufanya ili wasipotee. Leo tujifunze kupenda kupalilia neema za kubadilika, kutobaki katika dimbwi la ubaya/dhambi, tujitambue na kumkiri Kristo.

SALA: Ee Yesu utujalie neema ya kukutambua.