Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/04/2024

2024 APRILI 1 : JUMATU YA PASAKA

Mt. Hugo, Askofu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Mdo 2:14, 22-32

Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya; Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulubisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; utanijaza fuhara kwa uso wako. Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi; yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.

Wimbo wa Katikati. Zab 16:1-2, 5, 7-11

“1. Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakumkimbilia wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu. (K)

“Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia wewe.”

2. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)

3. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu.
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
4. Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele. (K)”

Injili. Mt 28:8-15

Wanawake waliondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.

TAFAKARI

UKWELI NI UKWELI: Habari za ufufuko wa Yesu zilisambaa kwa haraka kutokana na mambo matatu. Mosi; Tabia ya wanawake, kwa kawaida wanawake ni watu wenye tabia ya kupokea jambo na kuliamini kwa haraka na kupenda kulisambaza kwa wengine kwa haraka, wanaume ni tafauti kidogo, hupenda kuulilza uliza kwanza. Ndio maana hawa tuliowasikia katika Injili mara moja hawakuchelewa kusambaza habari za Ufufuko wa Yesu. Pili; Ujasiri wa Petro kwa wale Wayahudi ulikuwa chachu nzuri kwa habari hii kusambaa. Tatu; Kitendo cha Wakuu wa Makuhani na wazee kutumia nguvu nyingi ili kufifisha ukweli huu wa ufufuko wa Yesu. Kuna jambo ambapo kadiri unavyojitahidi kutaka lisijulikane, ndivyo litakavyosambaa kwa haraka. Nguvu waliyotumia Wayahudi kufifisha habari za ufufuko wa Kristo, zilifanya habari hii izidi kuenea. Je tujiulize, tunashiriki vipi kumtangaza Kristo mfufuka kwa wengine? Je, tunakuwa motomoto katika kumhubiri Kristo?

SALA: Ee Kristo mfufuka, tujalie tusimamie ukweli wa ufufuko wako.