Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 31/03/2024

2024 MACHI 31 : JDOMINIKA YA PASAKA
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

“Ndugu zangu; Mkiwa mmefufuliwa na Kristo, yafuateni yaliyo juu,  Kristo aliko ameketi mkono wa kuume wa Mungu” -Kol 3:1

Somo 1. Mdo 10:34, 37-4

Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa wahai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

Wimbo wa Katikati. Zab 118:1-2, 16-17, 22-23

“1. Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele. 

(K) Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

2. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)

3. Jiwe walilokataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu. (K)”

Somo 2. Kol 3:1-4

Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.

Injili. Yn 20:1-9

Hata siku ya kwanza ya juma Maria Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa

Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.

 

TAFAKARI

“UFUFUKO WA KRISTO NI UTHIBITISHO YAKINI WA IMANI YETU
Leo duniani kote inasikika sauti: Aleluya, Kristo amefufuka kweli, Bwana wetu yu mzima! Ni Pasaka ya Bwana. Hii ni Sherehe kubwa katika imani yetu inayothibitisha mafundisho yote ya Kristo. Yeye ambaye alionekana kushindwa na mafundisho yake pamoja na yote aliyotenda kuonekana si kitu na kuishia kufa msalabani anauthibitisha ukuu wake kwa kuwa hai tena. Muujiza huu mkubwa unatia muhuri kwamba ni kweli amekuja kwa ajili ya kutukomboa sisi wanadamu. Yote aliyotufundisha na kututaka tuyafanye ni kweli kabisa. Muujiza huu mkubwa unaelezewa na Antifona ya mwanzo ya sherehe hii kama maarifa ya ajabu: “Nimefufuka na ningali pamoja nawe; unmeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, Aleluya!”
Ufufuko wa Kristo ni ushindi dhidi ya dhambi. Uzima unashinda mauti. Dhambi ilipoingia duniani mwanadamu alifanywa mfu, uzima wa kimungu ulipotea ndani mwake. Mwanadamu alibaki akitawaliwa na mambo ya chini, mambo ya ulimwengu. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai unatuonesha mabadiliko hayo. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu siyo yaliyo katika nchi.” Mambo hayo ya chini, yaliyo katika nchi ndiyo mienendo ya kibinadamu, mambo ya giza ambayo yamemwingiza mwanadamu katika kifo cha kiroho. Ufufuko wetu katika Kristo unaonekana katika uhai, uhai ambao unathibitishwa na matendo yanayomshuhudia Kristo.
Dhambi ilimjengea mwanadamu kiburi na kujiona yupo sawa na Mungu na hivyo hakumwitaji Mungu. Hapa mwanadamu aliingia katika ulimwengu wake binafsi na kujiwekea taratibu zake ambazo hazikutilia maanani. Kiumbe alijifanya mmiliki wa uumbaji wote; tone la maji lilijikinai kuwa ni bahari nzima. Matokeo yake ni mfadhahiko katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu ambaye ameumbwa kama nafsi huru kabisa alijitengenezea ulimwengu wake na kwa kigezo cha uhuru huu kila mmoja alijifanya ni mkuu wa ulimwengu wake. Hapa pakazaliwa huria ya maadili; jamii ya mwanadamu ikajipeleka katika anguko kwa kukosa njia moja ya kuwaelekeza. Kristo alipokuja duniani akanuia tangu mwanzoni kurekebisha hili na kuirudisha hali ya mwanzo, yaani kuustawisha ufalme wa Mungu.
Mtume Petro na Yohane ambao walikwenda haraka kaburini baada ya kupokea taarifa ya Maria Magdalena walishuhudia kweli kaburi li tupu. Kwa Petro haikuelezwa sana. Injili inasema kwamba alivitazama na yule mwanafunzi mwingine yeye aliingia “akaona na kuamini.” Lakini ushuhuda anaoutoa Petro katika somo la kwanza unaielezea imani yake juu ya ufufuko wa Bwana. Tena anaunganisha tukio hili na maisha yote ya Kristo na yote yaliyompata tangu Galilaya hadi Yerusalemu. Kaburi lililo wazi bila shaka liliamsha dhamiri zao na akili zao na kukumbuka maneno yake kwamba “imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi na kuuwawa, na siku ya tatu kufufuka” (Mt 16:21). Kipindi kile Petro hakuelewa lakini sasa alipoingia kaburini na kumkuta hayupo akapata hakika yake.
Imani hii ya ufufuko wa Kristo inayapatia nguvu mafundisho yake yote. Katika hali aliyokuwa nayo Petro na wanafunzi wengine walijiona kuwa wamecheza mchezo wa pata potea. Yote aliyoyafundisha na kuyatenda kama muongozo kwa maisha yetu wanadamu yalipoteza ladha. Mwanzoni waliamini na kuona kweli mkono wa Mungu upo pamoja naye lakini ilikuwa ni vigumu kuuona uwezo wa Mungu unaoruhusu «Mwana wake mpendwa» kuuwawa tena katika namna ya aibu sana. Taa ilizimika ghafla. Tukio la ufufuko linaamsha tena matumaini mapya na nguvu mpya na linakuwa mwanzo wa maisha mapya. Petro anasema wazi kwamba yote tumeyaona tangu mwanzo hadi ufufuko wake; yote hayo tumeshuhudia na sasa sisi tunakuwa mashahidi wake.
Sherehe ya Pasaka inatualika katika maisha ya ushuhuda; inatualika kushuhudia kuwa kweli Kristo amefufuka. Hii inamaanisha tunapaswa kuonesha katika ulimwengu huu maana ya Ufufuko wa Kristo na jinsi unavyomwokoa mwanadamu. Zaburi imemtaja Kristo kama jiwe lililokataliwa na waashi ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la pembeni. Hapa tunaweza kuchota kitu cha kujifunza katika maadhimisho yetu ya mwaka huu, mintarafu hali halisi ya mwanadamu katika jamii. Tuutafakari ubinadamu ambao unadhalilishwa na dunia ya leo. Waashi wanaomkataa Kristo wanaonekana katika wakuu na wenye mamlaka wanaounda ulimwengu wetu wa leo. Hawa wametawaliwa na utamaduni wa kifo na kutupa nje jalalani kile kisicho na faida. Matokeo yake ni kuididimiza au kuififisha hadhi ya mwanadamu.
Kristo anayekataliwa anaonekana katika nafsi za wajane, yatima, wakimbizi, maskini, na watu wengine wengi walio wanyonge. Katika jicho la kibinadamu linalotawaliwa na waashi wa ulimwengu huu huonekana kuwa si kitu cha thamani kwani hawana mali, hawana mamlaka yoyote ya kijamii na katika ujumla wake hawana faida yoyote. Waashi hawa wa ulimwengu huu hawana upendo wa kimungu na hivyo ni aghalabu kuiona hadhi ya kaka au dada yake anayenyanyasika pembeni yake. Hivyo tunashuhudia matendo ya rushwa, unyonyaji, kupora haki za watu, vita, magonjwa, chuki za kindugu na mengineyo mengi. Hawa ambao wanakataliwa na waashi wanamwakilisha Kristo aliyekataliwa na nguvu za ulimwengu huu.
Mwaliko wa ushuhuda wa maisha ya ufufuko yanatupeleka katika furaha ya kweli. Sisi Wakristo tunaalikwa kushuhudia furaha hiyo kwa kumfanya Kristo kuwa jiwe kuu la pembeni. Falsafa ya jiwe la pembeni inaonesha umuhimu wake katika uimara wa jengo zima. Bila uwepo wa jiwe hili ambalo kwa kawaida huwa limepunguzwa kutoka sehemu kubwa jengo lote huwa katika hali ya udhaifu. Ndivyo unavyokuwa ubinadamu wetu unaoshindwa kuiona sura ya Kristo katika jirani anayeteseka. Tunapokuwa tayari kukunjua mikono yetu na kuwapokea, kuwasafisha na kuwaganga; tunapowarudishia hadhi yao na kuwapatia haki yao hapo tunaiokoa iliyo sehemu muhimu katika ubinadamu wetu ambayo bila hiyo tunabaki kuwa dhaifu. Hii ni kwa njia ya kuustawisha upendo wa Kristo mfufuka unaofumbata fadhila zote za kikristo.
Tukumbuke daima kwamba ufufuko wa Kristo ndiyo msingi wa maisha yetu ya imani. Tunapoichakachua furaha ya ufufuko wa Kristo kwa maisha ya dhambi tunapoteza ladha ya maisha yetu kiimani. Bwana amefufuka kwelikweli, Aleluya! Ufufuko wake unatia muhuri kazi yake yote ya kuukarabati ubinadamu uliochakazwa na dhambi. Tunapoishi katika ufufuko tunatembea katika nuru yake. “

SALA: Ee Kristo Mfufuka utujalie tufufuke pamoja nawe.