Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 11/03/2024

2024 MACHI 11 JUMATATU: JUMA 4 LA KWARESIMA
Mt. Teresa Margaret Redi 
Urujuani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. Isa 65:17-21

Bwana asema: ”Tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha. Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. 

Wimbo wa Katikati. Zab 30:2, 3-5, 11-13

1. Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni. (K)

(K) Nitakutukuza, ee Bwana, kwa maana umeniinua.

2. Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Na kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)

3. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)

Injili. Yn 4:43-54

Wakati ule, Yesu aliondoka Samaria, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipofika Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na  kumponya mwanawe; Kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, ”Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?” Yule diwani akamwambia, ”Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu.” Yesu akamwambia, ”Enenda; mwanao yu hai.” Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile alipoambiwa na Yesu, ”Mwanao yu hai.” Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake. Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.

TAFAKARI

MAZOEA HUJENGA KILEMA: Ukichunguza maisha ya viumbe kama Punda, Nyumbu, Panya n.k wanavyopita eneo moja mara nyingi hujenga mazoea na hata wanapokuwa wanapita huweza hata kupinda kona bila kuangalia kwa jinsi walivyozoea. Hii ni kutokana na mazoea ya muda mrefu. Hata mwanadamu ana hulka ya namna hii, anapokuwa mara kwa mara anafanya jambo, hujenga mazoea na wakati mwingine huishia katika dharau, kutotoa heshima stahiki na kujisemea, ‘oh huyu si nilikuwa nae jana! huyu si nilisoma nae! huyu si mtoto wa fulani! Hii inachangiwa na watu kumjua mhusika kwa undani hivyo kwamba wanavyojenga dharau hata akisema jambo zuri linapuuzwa. Mfano; Padre anaweza akaanza kuhamasisha waamini ili wajenge kanisa zuri lakini usishangae wakaanza kumbeza kwa kusema, ‘mbona kwao tunakufahamu, hamna hata nyumba nzuri!’ wazo lake litapuuzwa wala halitatiliwa maanani. Yesu akasema “Nabii hapokelewi kwao” Je mara ngapi tumekwamisha maendeleo ya Kanisa kwa kubeza wahusika kisa tunawafahamu?

SALA: Bwana tunakuomba utujalie neema ya kupokeana katika maisha yetu na kukubali mawazo ya wengine.