Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa 10/03/2024
2024 MACHI 10 JUMAPILI: DOMINIKA 4 YA KWARESIMA
Urujuani
Zaburi: Juma 4
Somo 1. 2Nya 36 :14-16, 19-23
Wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu. Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.
Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi; ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.
Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa Mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.
Wimbo wa Katikati. Zab 137:1-6
1. Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,
Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
Katika miti iliyo katikati yake
Tulivitundika vinubi vyetu. (K)
(K) Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa changu, nisipokumbuka.
2. Maana huko waliotuchukua mateka
Walitaka tuwaimbie;
Na waliotuonea walitaka furaha;
Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.(K)
3. Tuuimbeje wimbo wa Bwana
Katika nchi ya ugeni?
Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe,
Mkono wangu wa kuume na usahau. (K)
4. Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Nisipoikuza Yerusalemu
Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (K)
Somo 2. Efe 2 :4-10
Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda: hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
Injili.Yn 3 :14-21
Yesu alimwambia Nikodemo: Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
Na hili ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.
TAFAKARI
WEMA WA MUNGU HAUSHINDWI NA UOVU WA MWANADAMU: Mungu amemuumba mwanadamu kusudi aunganike naye milele. Hii ni kwa sababu ya upendo wake mkubwa usio na mwisho. Mwanadamu anapoingia katika hali ya uasi Mungu anaendelea kumfikiria na kumtafuta. Pamoja na kwamba wakati mwingine Mungu humwadhibu mwanadamu kwa sababu ya uovu wake, hukumu yake haiushindi upendo wake. Ndiyo maana Mama Kanisa anatupatia fursa kila mwaka ya kupita katika kipindi cha toba kusudi kustahilishwa kushirikishwa furaha ya upendo wake. Antifona ya Mwanzo ya Dominika hii inayoitwa Dominika ya Furaha inatualika katika furaha hiyo ikisema: “Furahi Jerusalemu: mshangilieni ninyi nyote mmpendao: furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake”. Tunaalikwa kufurahi sababu katika Yeye tutafarijiwa, tutanyonya maziwa na kushibishwa, ishara ya kuwa hai tena.
Somo la kwanza linatuonesha kuwa hukumu ya Mungu ni ya haki sababu ya uovu wetu; haki ya hukumu yake inaambatana na huruma yake, ufunuo wa upendo wake usio na kikomo kwani wema wake haushindwi na uovu wa mwanadamu. Dhambi zetu haziufifishi wema wake wala kumfanya Yeye kukata tamaa. Hii ni kwa sababu upendo wake mkuu wadumu milele. Mwenyezi Mungu aliwatumia wakuu wa wote na makuhani wa taifa ya Israeli wajumbe ili kugeuza mienendo yao “kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponywa”.
Mwanadamu katika hali ya uhasi mkuu hivi anatangaziwa wokovu wa Mungu kupitia Koreshi mfalme wa Uajemi. Hapa ndipo urefu na upana wa upendo wa Mungu unapojidhihirisha. Maneno yake kupitia kinywa cha Nabii anasema: “Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? … si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake akaishi?” (Eze 18:23). Mungu hafurahii hali yetu ya uovu. Hii ni kwa sababu sisi tulio matunda ya kazi yake njema ya uumbaji ametuumba tukiwa wakamilifu na wenye sura na mfano wake. Hali ya dhambi inatuziba na kushindwa kuionesha haiba hii; inaturubuni tuache kuutangaza ukuu wa Mungu unaofichika ndani mwetu.
Kilele cha upendo wake huu mkuu ni katika nafsi ya Kristo, mwanaye mpendwa, Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu sana. Yeye analetwa kwetu kama njia ya wokovu ambayo kwayo wote watakaomwamini wataokolewa. Kristo anaonesha namna ya kuujongea wokovu huo. Anamwambia Nikodemo katika somo la Injili: “Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.” Mwana wa Adamu atainuliwa juu msalabani ishara ya wokovu wetu. Tendo hili la kuinuliwa kutoka katika ardhi ni ishara ya kuinua macho ya mioyo yetu kutoka maisha ya kawaida ya dunia hii na kwenda juu.
Kuwa juu ni ishara ya kuungana na Mungu na kuyatazama malimwengu katika jicho la kimungu. Hiyo ndiyo imani ambayo Kristo anatualika tuwe nayo katika Yeye. Maisha yake ya hadharani hapa duniani yametufunulia namna mbalimbali za kuyakabili maisha katika jicho la Mungu. Ni wazi kwamba namna hiyo kwa walioangalia katika jicho la kidunia waliona ni chukizo kiasi cha kumwadhibu kwa namna hiyo ya kikatili. Lakini namna yao ya kumwadhibu kwa kumwinua juu ya msalaba ni sababu ya wokovu wetu na ufunuo wa upendo wa Mungu kwetu. Tunapoelekeza macho yetu katika msalalaba na kuungana naye huku tukiyaangalia malimwengu kutoka juu tutapata nguvu ya kupita katika ulimwengu kinzani huku tukielekea kwa Mungu.
Injili Takatifu inataadharisha pia juu ya upande wa pili, yaani kwa wale wasioamini. Neno la Mungu linasema: “asiyeamini amekwisha hukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” Asiyeamini ni yeye ambaye hapandi pamoja na Mwana pekee wa Mungu juu msalabani na kuyaangalia mambo katika namna ya Mungu. Huyu ni yule ambaye anatawaliwa na mienendo ya ulimwengu mamboleo ambao unaendelea kumpatia mwanadamu mwenye ukomo wa uelewa matumaini bandia juu ya ujuzi wake. Hukumu inamjia kwa sababu “nuru imekuja ulimenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.” Mwanadamu anayeacha kumtazama Yeye aliyeinuliwa juu msalabani anaishia katika giza kwa sababu anabaki katika ukomo wa kuona ukweli wote.
Mwanadamu ana ukomo katika uelewa wake. Hivyo ni pale tu mwanadamu anapounganika na Mungu mwenye uwezo wa kujua na kuona yote ataweza kufanikiwa. Leo hii tunashuhudia jamii ambayo haitaki kuinua macho juu na kuyaelewa yote katika muono wa kimungu. Matokeo yake tunakuwa ni kizazi chenye uelewa nusunusu wa mambo mbalimbali yamhusuyo mwanadamu. Masuluhisho mengi hufanyika nusunusu na wakati mwingine kutawaliwa na ubinafsi au kutafuta maslahi ya mtu mmoja mmoja. Kila mmoja anakuwa ni mjuaji na matokeo yake ni mafarakano na kutoelewana kati yetu. Hatuwezi kamwe kutoka katika hali hii kama tusipoitazama hii nuru inayotuzukia katika Yeye aliyeinuliwa juu msalabani.
Mtume Paulo anatukumbusha haiba yetu kwamba “tumeokolewa kwa neema.” Hali hii ya neema inatutenga na ulimwengu na kutuunganisha na Kristo aliyeinuliwa msalabani. Ni zawadi ya Mungu kwetu anayotupatia bila hata kustahili. Hii ni kwa sababu hata tulipokuwa katika hali ya dhambi kwa mastahili yetu “alituhuisha pamoja na Kristo.” Sakramenti ya ubatizo inatupatia uzima mpya. Tunazaliwa mara ya pili na kujazwa neema ya Mungu ndani mwetu, neema ambayo inatufanya kuwa wana warithi wa Mungu. Mwitikio wetu unapaswa kuwa ni shukrani kwa Mungu. Mzaburi anatuonesha namna njema ya kushukuru kwa njia ya kuyakumbuka matendo ya Mungu. Israeli alipokumbuka hali yake akiwa utumwani Babeli na hali yake ya sasa katika uhuru anaimba kwa shukrani akisema: “Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka”
Kipindi cha Kwaresima ni fursa nyingine kwetu ya kubadili mwelekeo wa maisha kwa ajili ya wokovu wetu sote. Tuikumbuke aiba yetu kwamba tumeinuliwa juu kutoka katika ulimwengu huu. Ni kipindi ambacho tunaalikwa kuyainua macho yetu juu na kuelekeza kwa Mungu kwa kumtazama Yeye waliyemchoma. Kwake tunaweza kumwona Mungu ambaye amejinyenyekesha katika namna ya ajabu kwa ajili ya wokovu wangu mimi na wewe. Msalabani anatufundisha unyenyekevu, msamaha, utii, uvumilivu na zaidi ya yote upendo fadhila ambazo kwazo zinaimarisha mahusiano yetu na Mungu na pia mahusiano yetu sisi kwa sisi. Tendo letu la kumtazama Kristo msalabani litaufunua upendo wa Mungu na hivyo tunafanywa kuwa sababu ya wokovu kwa ulimwengu wote. Upendo wa Mungu kwetu ni mkubwa mno na kamwe haushindwi wala kufifishwa na uovu wa mwanadamu.
SALA: Ee Bwana utujalie neema ili macho yetu yaelekee zaidi upendo wako.