Select Page

Tumsifu Yesu Kristu… Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 25/02/2024

2024 FEBRUARI 24: DOMINIKA YA 2 YA KWARESIMA
Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mwa 22 :1-2, 9a, 10-13, 15-18

Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketeza badala ya mwanawe. Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno  hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga uliopo pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

Wimbo wa Katikati. Zab 116: 10,15-19 

1. Naliamini, kwa maana nitasema,
Mimi niliteswa sana.
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.  (K)

(K)  Nitaenenda mbele za Bwana  Katika nchi za walio hai. 

2. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
Umevifungua vifungo vyangu.
Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)

3. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Katika nyua za nyumba ya Bwana,
Ndani yako, Ee Yerusalemu. (K)

Somo 2. Rum 8 :31b-34

Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajii yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.

Injili. Mk 9 :2-10

Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohane, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikua wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.

TAFAKARI

Ni Dominika ya pili ya Kwaresima. Wazo kuu ni “Kusikiliza na Kutii.” Wazo hili linapatikana katika somo la kwanza na lile la Injili. Katika somo la kwanza (Mwa 22:1-2, 9a, 10-13, 15-18), tunasikia kisa cha Ibrahimu akiombwa na Mungu amtoe sadaka mtoto wake pekee, Isaka. Ibrahimu anaambiwa: “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kutekezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia”(Mwa 22:2). Ibrahimu akaisikiliza sauti hii ya Mungu, akamtii. Hivyo akamchukua Isaka hadi mlimani. Na mara walipofika pale Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Kitendo hiki cha Ibrahimu kumsikiliza Mungu na kuitii sauti yake kilimpelekea Mungu kumpatia Ibrahimu kondoo kama mbadala wa Isaka. “Ibrahimu! Ibrahimu! Usimnyonyeshee kijana wako mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa najua kwamba unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia nwanao, mwanao wa pekee.”(Mwa 22:12). Na mara Ibrahimu akageuka nyuma akaona kondoo mume. “Akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketeza badala ya mwanawe”(Mwa 22:13).
Simulizi hii ya Ibrahimu inatupatia maswali mawili matatu. Moja, imewezekanaje Mungu kumpa Ibrahimu ombi gumu kiasi kile? Ikumbukwe kwamba Isaka alikuwa mwana wa ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu na Sara. Hivyo kumwomba Ibrahimu amtolee sadaka Isaka lilikuwa ni jambo ambalo kibinadamu lilikuwa gumu kulitekeleza. Pili, imewezekanaje Ibrahimu akakubali ombi la Mungu pasipo kuuliza lolote? Ikumbukwe kwamba Isaka kwa Ibrahimu ndiye alikuwa mrithi wa ile ahadi ya Mungu aliyompatia Ibrahimu wakati akimwita atoke katika nchi yake (Mwa 12:1-3). Hivyo kumtoa Isaka sadaka ni kutotimia kwa ahadi zile. Tatu, imewezekanaje kwamba Isaka, kijana mdogo lakini aliyekuwa na uwezo walau hata kukimbia ili kukwepa kutolewa sadaka, na hasa pale mzee Ibrahimu aliponyosha mkono wake na kutwaa kisu ili amchinje?
Maswali haya na mengineyo yanatupelekea kutambua kwamba kulikuwa na uhusiano wa kipekee kati ya Mungu na Ibrahimu. Uhusiano huu ulijengwa juu ya imani. Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anaonyesha uhusiano huu anapoandika kwamba “Kwa imani Abrahamu alimtoa dhabihu mwanawe Isaka wakati Mungu alipomjaribu. Huyo Abrahamu ndiye aliyekuwa amempokea ahadi ya Mungu, lakini, hata hivyo, alikubali kumtoa dhabihu mwanawe wa pekee, ingawa Mungu alikuwa amemwambia: ‘Wazao wako watatokana na Isaka…'”(Ebr 11:17-19).
Hii ni Kwaresima. Simulizi hili la Ibrahimu linatupatia sisi swali la jinsi tunavyotimiza moja ya masharti ya Kwaresima: Kutoa sadaka. Kutoa sadaka ni mojawapo ya nguzo tatu za Kwaresima. Nyingine ni Sala na Kufunga. Wengi wetu tu wagumu wa kujitoa sadaka na kutoa sadaka kwa sababu tunadhani tu-fukara. Tunasubiri tuwe na vya ziada ili kutoa sadaka. Tunaogopa kufilisika. Ibrahimu ni mfano wetu wa kujitoa na kutoa sadaka hata kwa kidogo tulicho nacho. Tuige pia moyo wa mama mjane maskini ambaye alitoa sadaka ya “Kila kitu alichohitaji kwa kuishi”(Lk 21:1-4). Mungu huwarudishia ukarimu walio wakarimu. Ndivyo inavyotokea katika maisha ya Ibrahimu, kwani Mungu anambariki Ibrahimu kwa kuzidisha uzao wake. Na sababu ni kwamba “Umetii sauti yangu”(Mwa 22:18). Kusikiliza ni kutii.
Katika Injili (Mk 9:2-10) wakati wa tukio la kung’ara sura kwa Yesu Kristo, sauti ya Mungu Baba inasikika ikituambia “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye”(Mk 2:7). Kuisikia sauti ya Yesu ni kuitii sauti yake. Na kuitii sauti yake ni kufuata masharti yake ya ufuasi. Mojawapo ni “Kujikana, kuchukua msalaba, kumfuata”(Mk 8:34). Ni kujitoa sadaka. Ni sadaka ile ya msalaba. Ni kujikatalia. Na hatuwezi kutimiza hayo bila kwanza kusikiliza na kuutii mwaliko wake.
Hii ni kwaresima. Tunapotafakari juu ya kujitoa kwetu sadaka, hatuna budi nasi kwenda mlimani kama alivyofanya Ibrahimu kule Moria na Yesu kule Tabor. Twende mlimani ili tukakutane na Mungu. Twende mlimani mahali pa sala. Twende mlimani tukamkabidhi Mungu maisha yetu yawe sadaka safi na ya kumpendeza. Twende mlimani tukauone utukufu wa Mungu kama vile Petro, Yakobo na Yohane walivyouona hata wakatamani kubaki pale. Twende mlimani ili tukajifunze sheria za Mungu na kuyasikiliza mafundisho ya manabii. Twende mlimani ili tukamsikilize Kristo na kumpa nafasi ya kutubadilisha maisha na kuyang’arisha kwa utakatifu wake.
 Hii ni Kwaresima. Tunapoanza juma la pili, tuombe neema ya usikivu na utii kwa neno la Mungu ili tuweze kujifunza kujitoa sadaka na kutoa sadaka kwa kidogo tulicho nacho kwani “Yeye (Mungu) ambaye alimtoa Mwanaye kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?”(Rum 8:32). 

SALA: Ee Bwana utujalie fadhila ya utii ili tuweze kuisikiliza sauti yako. Amina.