Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 13/02/2024

2024 FEBRUARI 13 JUMANNE: JUMA LA 6 LA MWAKA
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1:  Yak. 1: 12-18

Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.

Wimbo wa Katikati: Zab 94: 12-15, 18-19

1. Ee Bwana, heri mtu Yule amwadibuye na kumfundisha,
kwa sheria yako;
Upata kumstarehesha siku ya mabaya. (K)

(K) Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha. 

2. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake,
Wala hutauacha urithi wake,
Maana hukumu itarejea haki,
Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)

3. Niliposema, mguu wangu unateleza;
Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu,
Faraja zako zaifurahisha roho yangu. (K)

Injili. Mk 8: 14-21

Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?

TAFAKARI

TUWE WAANGALIFU KATIKA KUJARIBIWA: Uangalifu katika majaribu unatokana na uhalisia kuwa, kwa kukosa uvumilivu malengo hayatimii na kwa kuvumilia malengo yanatimia. Kadiri ya Yakobo astahimiliye majaribu atapokea taji ya uzima kutoka kwa Bwana. Majaribu huja kwa tamaa na tamaa huleta dhambi na dhambi huleta mauti. Tunayaona majaribu yaletwayo na tamaa kutoka kwa Mafarisayo na Herode katika Injili. Mafarisayo walimfikiria Masiya katika namna ya kutenda miujiza, kupambana, kuona maono, ushindi wa kitaifa na ukuu wa kisiasa, na Herode alijitahidi kupata furaha kupitia kutwaa madaraka, mali, ushawishi na sifa. Kwa wote, Mafarisayo na Herode, ufalme wa Mungu ulikuwa ni ufalme wa kiulimwengu, uliotegemea ukuu na nguvu za kidunia. Kwa wayahudi neno chachu liliashiria dhambi. Yesu alikumbuka kuwa ni muda mfupi tu Mafarisayo walimjaribu kwa kutaka ishara ya Mbinguni na alikumbuka majaribu na hila za Herode za kutaka kumuangamiza, hivyo aliwatahadharisha wafuasi wake kuwa makini nao kwani mienendo yao ni ya dhambi. 

SALA: Tunatambua nguvu na uwezo wako Bwana tunakuomba utuwezeshe kutambua majaribu na kukabiliana nayo kiimani, amina.