Select Page

Atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu. Karibu Katika Masomo ya Misa Takatifu 07/02/2024

2024 FEBRUARI 7 JUMATANO: JUMA LA 5 LA MWAKA

Kijani

Zaburi: Juma 1

SOMO 1:  1 Fal. 10: 1-10

Malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.

Wimbo wa Katikati. Zab 37:30-31, 39-40

1. Umkabidhi Bwana njia zako,
pia umtumaini naye atafanya.
Akaitokeza haki yako kama nuru,
na hukumu yako kama adhuhuri. (K)

(K) Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.


2. Kinywa cha mwenye haki hunena hekima,
na ulimi wake husema hukumu.
Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake,
hatua zake hazilegezi. (K)

3. Wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
huwaopoa wasio haki na kuwaokoa,
kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

Injili. Mk 7: 14-23

Yesu aliwaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.

TAFAKARI

MAOVU NI ZAO LA MOYO ULIOJAZWA UOVU: Katika maisha yetu, maovu tuyatendayo kimwili hayaanzii mwilini bali moyoni ambako maovu huchimbuka. Mwili hutekeleza kile kilichochakatwa moyoni. Katika mtazamo huo, tunamuona Yesu anarekebisha sheria ya kiyahudi iliyokataza watu kula baadhi ya vyakula wakiaminishwa kuwa ni najisi. Yesu anasisitiza kuwa hakuna kitu najisi au safi katika mtazamo wa kidini, ila mtu anatiwa unajisi kwa yale yanayomtoka, yaani matendo yake ambayo ni zao la moyo wake. Namna hii ndio tunayoshuhudiwa na Hekima ya Mfalme Sulemani. Mfalme huyu baada ya kujaribiwa na Malkia wa Sheba ambaye alisikia habari zake, hakuzalisha chuki, hakuzalisha uovu wowote mbaya bali hekima iliyodhihirishwa na majibu yake kwa Malkia. Wapendwa katika Kristo, tunakumbushwa juu ya matokeo ya matendo yetu, tunapotenda vema tunaashiria kuwa tuliyonayo moyoni pia ni mema, na tunapotenda dhambi tunadhihirisha kuwa ndani ya mioyo yetu tunajenga mazingira ya dhambi. Daima tunapaswa kujikita kuzifanya dhamiri na mioyo yetu kuwa katika hali njema kwani kutoka kwazo tunatenda.

SALA: Ee Mungu, tunakuomba utuongoze daima tuijaze mioyo yetu mambo yaliyo mema kwani tunapoijaza mawazo maovu tunakukosea wewe, amina.