Select Page

Tumsifu Yesu Kristu. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/01/2024

2024 JANUARI 30 JUMANNE: JUMA LA 4 LA MWAKA

Mt. Gilberti, Padre

Kijani

Zaburi: Juma 4

SOMO 1:  2 Sam. 18: 9-10. 14b, 24-25a. 30 – 19: 3

Kwa bahati Absalomu alikutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele. Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, “Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni.” Yoabu akachukua vyemba vitatu mikononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni.   Basi Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili; mlinzi akapanda juu hata dari la lile lango hata ukutani, akainua macho yake, akaangalia, na tazama, mtu anakuja mbio peke yake. Mlinzi akalia, akamwambia mfalme, Naye mfalme akasema, “kama yu peke yake, ana habari kinywani mwake.” Akaja mbio, akakaribia. Naye mfalme akasema, “geuka, usimame hapa.” Akageuka, akasimama.   Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, “nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana Bwana amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe.” Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, “yule kijana, Absalomu, je! Yu salama?” Yule Mkushi akajibu, “Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana.” Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, “Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!”   Kisha Yoabu akaambiwa, “Angalia, mfalme anamlilia Absalomu na kumwombolezea.” Na kushinda kwao vitani siku ile kukageuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote; maana watu walisikia siku ile ya kwamba, “Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.” Watu wakajificha siku ile, wakaingia mjini kama vile watu waonao fedhea wajifichavyo, hapo wakimbiapo vitani.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 86: 1-6

Ee Bwana, utege sikio lako unijibu Maana mimi ni maskini na mhitaji. Unihifadhi nafsi yangu maana mimi ni mcha Mungu,Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.

(K) Ee Bwana, Utege sikio lako, unijibu.

Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia mchana kutwa. Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia wewe, Bwana. (K)

Kwa maana wewe, Bwana, u mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao. Ee Bwana, uyasikie maombi yangu, Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)          

INJILI:  Mk. 5:21-43

Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, “Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi.” Akaenda pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga songa. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.” Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, “Ni nani aliyenigusa mavazi yangu?” Wanafunzi wake wakamwambia, “Je! Wawaona makutano wanavyokusonga songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa?” Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.” Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, “Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?” Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, “Usiogope, amini tu.” Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, “Mbona mnafanya ghasia na kulia?” Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, “Talitha, kumi;” tafsiri yake, “Msichana, nakuambia, Inuka.” Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.

TAFAKARI

KWA IMANI TUNATIMIZIWA HAJA ZETU: Imani ndiyo dira msingi ya maisha yetu hususani katika mapambano ya maisha yetu. Maishani tunapambana ili tutimize haja zetu. Katika Somo la kwanza, twaona Mfalme Daudi amekuwa akipitia kipindi kigumu kwani mwanae amekuwa akimtafuta amwangamize. Kwa imani yake Daudi anatambua kuwa atamshinda adui yake kwa uwezo wa Mungu, hivyo anamuachia Mungu, na baadaye adui yake anashindwa. Katika Injili, Yairo, Mkuu wa Sinagogi mwenye mtoto anayeumwa karibia kufa, na mwanamke aliyetokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, wanasaidiwa haja zao kila mmoja kadiri ya uhitaji wake. Wanasaidiwa kwa kuwa wana imani kwa Yesu ya kwamba haja zao zitatatuliwa naye. Wapendwa Taifa la Mungu, haja za maisha yetu zinatatuliwa kwa kuwa na imani thabiti kwa Yesu. Hakuna tatizo kubwa linalozidi uwezo wa Mungu. Tukiamini kuwa Kristo atatutimizia haja zetu daima tutamtafuta na kumwomba atusaidie.

SALA:Ee Mungu tujalie kutambua kuwa bila imani kwako hatuwezi lolote, tuongoze daima tuifuate vema imani yetu tukitambua kuwa haja zetu zinatimizwa kwa imani hiyo, amina.