Select Page

Kristu Jana. Karibu katika Masomo ya Misa Takatifu 23/01/2024

2024 JANUARI 23 JUMANNE: JUMA LA 3 LA MWAKA

Kijani

Zaburi: Juma 3

SOMO I:  2 Sam. 6:12-15, 17-19

Daudi alienda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la Bwana walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng’ombe na kinono. Daudi akacheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la Bwana kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.   wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabariki watu kwa jina la Bwana wa majeshi. Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake.

WIMBO WA KATIKATI:              Zab. 24:7-10

Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia.

(K) Ni nani mfalme wa utukufu?

Ndiye Bwana, Mfalme wa utukufu. Ni nani mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu hodari, Bwana hodari wa vita. (K)

Inueni vichwa, enyi malango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K)

Ni nani huyu wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye  ndiye mfalme wa utukufu. (K)

INJILI:  Mk. 3:31-35

Walikuja mamaye na nduguze wa Yesu; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka; wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu yeyote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.

TAFAKARI

UNDUGU WA KWELI UPO KATIKA KUTIMIZA MAPENZI YA MUNGU: Wapendwa Taifa la Mungu, Undugu wa kweli unatuletea amani, furaha na faraja kwasababu unatimia kwa kufuata mapenzi ya Mungu. Daudi na nyumba yote ya Israeli wanafurahi kwa kulirejesha Sanduku la Mungu kwao. Wanafurahi kwa kuwa Agano lao na Mungu limerejea tena. Furaha hiyo inaendeleza undugu wao na Mwenyezi Mungu. Kwa kufuata na kuishi Agano lao na Mungu ambalo ndio muungano wa kindugu, wanatekeleza na kutimiza mapenzi ya Mungu. Bwana Yesu Kristo hawakatai ndugu zake, bali anasisitiza kuwa undugu wa damu pekee hautoshi, undugu unapaswa kutimiza matakwa ya Mungu. Undugu unaotimiza mapenzi ya Mungu unachochea upendo, kusaidiana, kusikilizana, kushauriana kindugu, kuishi pamoja, hata kufarijiana pia. Undugu wetu wa kibinadamu unachangamoto nyingi, umejaa udanganyifu, masengenyo, unafiki, tena ni wa mda mfupi tu. Lakini undugu wa Kimungu hauna kikomo na hutuletea furaha ya milele.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utujalie moyo wa kujaliana kindugu kadiri ya mpango wako, utufanye daima tuwe na shauku ya kuyatimiza mapenzi yako, amina.