Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 17/09/2024

2024 SEPTEMBA 17: JUMANNE-JUMA LA 24 LA MWAKA

Mt. Roberto Belarmino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma IV

SOMO 1. 1 Kor 12:12-14, 27-31

Kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinywesha Roho mmoja.  Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 100: 1b-5

1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.

(K) Tu watu wake na kondoo wa malisho yake.

2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)

4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

INJILI. Lk 7:11-17

Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kandokando.

TAFAKARI

TUWE FARAJA KWA WENGINE: Fikiria juu ya maisha ya huyu mama mjane, kumpoteza mwanawe wa pekee. Kwenye mila na desturi nyingi ni tendo la huzuni sana linahitaji kuonewa huruma sana. Kristo aliposogea karibu naye alishikwa na huruma akaanza kumfariji huyu mama. Alipowafikia waombolezaji, waliokuwa na changamoto katika maisha aliwaelezea amezaliwa katika uzima mpya. Ishara hiyo ya maana zaidi katika maisha yetu inafungamanishwa na imani kwa Kristo ambaye ni uzima na ufufuo wetu. Hakujali kuwa kwa asili akigusa jeneza anajitia unajisi bali akisukumwa na huruma na kumfariji mama mjane na waombolezaji, analigusa jeneza na kumrudishia kijana uhai. Hakika ulikuwa ni wakati wa furaha kubwa lakini pia mshangao kwa watu, inawezekana je jambo hili? Kama Wakristo tujifunze nini kwenye tukio kama hilo: Tuwaonee huruma wale wanaoteseka na kufikwa na majanga ya namna mbalimbali.  

SALA: Ee Bwana Yesu utufanye tuwe vyombo vyako vya faraja kwa wenye dhiki mbalimbali.