Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 20/09/2024
2024 SEPTEMBA 20: IJUMAA-JUMA LA 24 LA MWAKA
Mt. Andrew Kim Taegon, Padre na Shahidi, Paul Chong Hasang
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma IV
SOMO 1. 1 Kor 15: 12-20
Ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka! Tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa oungo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 17: 1, 6-8, 15
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, (K) Nishibishwe, Ee Bwana, kwa sura yako. 2. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, 3. Unilinde kama mboni ya jicho lako, |
INJILI. Lk 8: 1-3
Yesu alikuwa akizungukazunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao. |
TAFAKARI
TUWE KARIBU NA KRISTO: Sehemu ya Injili inamuonesha Kristo akiendelea na utume wake wa kuwahudumia watu kwa kuwafundisha, kuwaponya, kutoa pepo na kuutangaza ufalme wa Mungu. Pamoja na Kristo waliandamana naye wale mitume kumi na wawili na baadhi ya wanawake. Hivi inaonesha kuwa katika kazi zake za ukombozi wa ulimwengu, Kristo alipenda hawa wafuatane naye ili waendelee kujifunza kwake na wengine waliendelea kumtumikia na kuhudumia kwa mali yao wenyewe. Tunajifunza Kristo anawaita watu wote kuwa wanafunzi na mitume wake bila ubaguzi wowote. Paulo Mtume ni mmoja wa walioteuliwa bila kutarajia anatetea matumaini yetu katika ufufuko wa wafu ambapo msingi wake ni ufufuko wa Kristo Mwenyewe. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo ametufungulia mlango wa kushiriki utukufu wa Mungu Baba. Shughuli nyingi na vitu vingi vya maisha ya sasa wakati mwingine vinatufanya tunapoteza lengo letu la kuwa karibu na huo ufalme wa Mungu. Tukimfuata Kristo kwa ukaribu tutakuwa na ufahamu sahihi wa ufalme wa Mungu na hivyo kushuhudia kwa ujasiri. SALA: Ee Bwana utujalie siku zote kuandamana nawe katika maisha yetu. |