Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/09/2024

2024 SEPTEMBA 21: JUMAMOSI-JUMA LA 24 LA MWAKA

MT. MATHAYO, MTUME NA MWINJILI
Rangi: NYEKUNDU

Zaburi: Tazama Sala ya Siku

SOMO 1. Efe 4:1-7, 11-13

Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, Imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wenu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 19:2-3, 4-5

1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yako.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.

(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.

2. Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)   

INJILI. Mt 9:9-13

Yesu alipokuwa akipita aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, “Nifuate.” Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Naye aliposikia, aliwaambia, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

TAFAKARI

TUSHIRIKIANE NA MPANGO WA MUNGU: Tunaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Matayo Mwinjili. Kabla ya kuongoka kwake Matayo, alikuwa ni mtoza ushuru katika pwani ya Galilaya. Siku moja alipokuwa akiendelea na shughuli zake za kawaida, Bwana Yesu alipokuwa akipita alimtazama akamwambia “nifuate.” Kinachovutia, Matayo aliacha kazi aliyoizoea yenye marupurupu na malipo ya fedha nyingi, hakuwaaga hata ndugu zake, akamfuata Yesu. Aliandaa karamu kubwa nyumbani akamwalika Kristo, wafuasi na marafiki wengine. Mafarisayo ambao hawakumpenda Yesu, hawakupendezwa na kitendo hicho chake kushiriki karamu hiyo. Wao waliwaona watoza ushuru kama wadhambi kuliko watu wengine. Wivu wao haukumfanya Kristo asiendele na kazi yake ya kumkomboa mwanadamu. Kama Matayo aliyeitikia Mwito Paulo anawahimiza Waefeso na sisi pia tuenende kama inavyoustahili wito wetu tulioitiwa na Mungu, kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, tukichukuliana kwa upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Tushirikiane na huo mpango wa Mungu.

SALA: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuipokea kwa furaha zawadi ya wito na kuuishi kwa kushirikiana na mpango wako wa ukombozi.