Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 16/09/2024

2024 SEPTEMBA 16: JUMATATU-JUMA LA 24 LA MWAKA

Mt. Korneli, Papa na Sipriano Askofu, mashahidi
Rangi: Nyekundu

Zaburi: Juma IV

SOMO 1. 1 Kor 11:17-26, 33

Katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojane.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 40:7-9, 17

1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.

(K) Mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

2. Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu
Naama, sheria yako ime moyoni mwangu. (K)

3. Nimehubiri habari za haki katika kuanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)

4. Washangilie, wakafurahie,
Wote wakutafutao.
Waupendao wokovu wako
Waseme daima, Atukuzwe Bwana. (K)

INJILI. Lk 7:1-10

Yesu alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni kwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.

TAFAKARI

TUISTAWISHE ZAWADI YA IMANI: Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Zawadi ya Imani inaweza kulinganishwa na zawadi ya mbegu anayoweza kupewa mkulima. Mkulima anaweza kuleta gunia moja au magunia mia moja. Mungu ni mkarimu anamgawia kila mmoja kwa kadiri alivyo tayari kupokea zawadi hizo. Kwani hata mkulima anapopokea mbegu akienda nayo nyumbani anaweza kuamua akaziotesha na kupalilia au anaweza kuotesha bila kuitunza au anaweza kuitunza hadi ikaharibika au mwingine asiitoshe akaitumia kama chakula. Tunasema “ukarimu huzaa ukarimu.” Tukitoa au kupokea kwa ukarimu tunazidishiwa. Tunapojitahidi kuistawisha na kuitunza zawadi ya imani tuliyoipokea inastawi zaidi. Huyu jemedari ameonesha ukarimu wa juu sana kwa kumjali mtumishi wake. Amewashirikisha wazee wa kiyahudi lakini pia amedhihirisha anaipenda imani kwa kuwatuma wakamlete Kristo aje kumponya huyu mtumwa. Matendo yetu mema, huduma yetu ya ukarimu na huruma yetu kwa wengine siku moja yataturudia.

SALA: Ee Bwana tunaomba uendelee kutuzidishia zawadi ya imani tuendelee kushiriki matendo yako makuu.