Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 15/09/2024

2024 SEPTEMBA 15: DOMINIKA YA 24 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma IV

SOMO 1. Isa 50: 5-9

Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? na anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?

WIMBO WA KATIKATI. Zab 116: 1-6, 8-9

1. Aleluya.
Nampenda Bwana kwa kuwa ananisikiliza
Sauti yangu na dua zangu.
Kwa maana amenitegea sikio lake,
Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.

(K) Nitaenenda mbele za Bwana Katika nchi za walio hai.

2. Kamba za mauti zilinizunguka,
Shida za kuzimu zilinipata.
Niliona taabu na huzuni,
Nikaliitia jina la Bwana;
Ee Bwana, Mungu wangu, uniokoe. (K)

3. Bwana ni mwenye neema na haki,
Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema,
Bwana huwalinda wasio na hila,
Nilikuwa taabuni akaniokoa. (K)

4. Maana ameniponya nafsi yangu na mauti,
Macho yangu na machozi,
Na miguu yangu na kuanguka.
Nitaenenda mbele za Bwana
Katika nchi za walio hai. (K)

SOMO 2. Yak 2: 14-18

Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.  

INJILI. Mk 8: 27- 35

Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohane Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.  Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu.  Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

TAFAKARI

WEWE NI KRISTO
Neno Kristo linapata asili yake katika neno la kiyunani “khristos” ambalo ni tafsiri ya neno la kiebrania “masiah” linalomaanisha “Yule aliyepakwa mafuta”. Hivyo yeye aitwaye Kristo ni yeye anayepakwa mafuta na kutengwa kwa ajili ya kazi maalum ya Mungu. Biblia Takatifu wakati wa agano la kale imetuonesha mifano mbalimbali. Tuchukulie mathalani jinsi Daudi alivyopakwa mafuta ili kuwa Mfalme wa Israeli. Tukio zima lilionesha kuwa ni Uchaguzi wa Mungu: “Ondoka umtie mafuta; maana huyu ndiye” (1Sam 16:12). Kabla ya kuzaliwa kwa Kristo malaika alimtokea Mtakatifu Yosefu na kumwambia kuwa mtoto ambaye mkewe Mariamu ana mimba yake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ataitwa jina lake Yesu likimaanisha mwokozi (rej. Mt 1:23,25). Katika Injili ya leo Mtume Petro anamkiri Yesu kuwa ni Kristo yaani mpakwa mafuta wa Bwana. Tunapounganisha majina haya “Yesu” na “Kristo” tunaipata maana pana ya utume wake ambao kilele chake ni katika fumbo la msalaba.
Swali la Kristo kwa mitume wake linakuja wakati muafaka, siku mbili baada ya kuadhimisha Sikukuu ya kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu. Bila shaka Petro na wenzake walikwishatambua kuwa Yesu ni mteule wa Mungu hivyo hawakuwa na shaka kumtaja kama Kristo. Kristo analipokea jibu lake lakini Injili inaendelea kusema: “akawaonya wasimwambie mtu habari zake”. Pengine hatulitilii maanani onyo ili lakini lina maana kubwa kwani huyu mpakwa mafuta alitambua wazi umuhimu wa kusubiri ukamilifu wa Fumbo la Pasaka kwa ajili ya kueleweka vema. Hivyo si ajabu tunaona mara moja anamkaripia Petro. Kristo anadiriki kumuita Petro shetani: “nenda nyuma yangu shetani.” Shetani anatajwa hapa kama kikwazo cha utii wa mwanadamu wa kale kwa mwenyezi Mungu. Petro anapoambiwa anayawaza ya wanadamu inamaanisha ni yule mwanadamu wa kale ambaye alijiamuamulia kujitenga na Mungu, kufikiri yaliyo yake bila kumhusisha Mungu kwa kuitii sauti ya shetani.
Yesu Kristo ametengwa na Mungu kwa ajili ya kazi ya ukombozi wetu kwa kupitia njia ya msalaba. Yeye anaunganika na ubinadamu huu uliojitenga na Mungu; ubinadamu uliojiweka chini ya utii wa shetani ili kuukomboa na kuurudishia upya hadhi yake. Anauvaa ubinadamu wetu ili kutushirikisha umungu wake na katika muungano huo wa ajabu anatuonesha namna njema ya kuunganisha maisha yetu kiroho na kimaadili na mpango wa Mungu. Msalabani tunamuona Mungu anayedhalilika; tunauona ukuu unaodhihakiwa; tunauona utukufu unaochafuliwa. Lakini namna hii ndiyo inayomuokoa mwanadamu. Katika “kenosi” yake (rej. Flp 2: 6 – 8) Kristo anasema ndiyo kwa mapango wa Mungu. Ndiyo yake hii inampeleka katika ukuu: “Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina” (Flp 2:9). Fumbo la msalaba linaifunua haiba ya Kristo kama Mwana mpendwa wa Mungu. Yeye ameunganika na Mungu katika kifungo cha utii kisichofunguka kamwe katika upendo wa Roho Mtakatifu. Hiyo njia ya kuelekea wokovu, yaani kusema ndiyo katika mpango wa Mungu, kuunganikan naye milele.
Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatufunulia namna Yesu Kristo alivyokubali kulipokea fumbo la msalaba na kuikamilisha “kenosi” yake. Ni katika hali ya unyenyekevu. Hii namna ambayo anatufundisha sisi kwamba, ili kuweza kuyatimiza vema mapenzi ya Mungu tunapaswa kujitoa wazima wazima, kujisadaka nafsi na kumfanya Yeye mwenyezi atende ndani mwetu: “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma”. Mwenyezi Mungu ndiye anayetuwezesha kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kuipokea hali ya unyenyekevu mithili ya Kristo na kujiweka chini ya uangalizi wake. Kujikabidhi wazima mikononi mwa Mungu kunatanguliwa na muunganiko wetu na Yeye katika imani, muungano ambao unatufanya kumfahamu sawasawa na kuweka tumaini letu lote kwake. Namna hiyo inatuwezesha kupita katika hali zote za maisha bila kuacha kuelekeza macho yetu kwake. Katika raha na mafaniko hatutamdharau na kumwacha na katika shida hatutamlalamikia. Nabii Isaya anamalizia kwa kusema: “Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami?… Tazama Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?
Sisi Wakristo pia tunatengwa na Mungu. Tunakuwa wapakwa mafuta kwa ajili ya kazi ya Mungu. Sakramenti ya Ubatizo inatushirikisha hadhi hiyo na hivyo tunaunganishiwa tena uhai wa fumbo la Utatu Mtakatifu sana. Mkristo anaitwa mbeba Kristo na hiyo kama anavyotufundisha Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa pili kwamba mkristo anapaswa “kujishikamanisha na nafsi ya Kristo mwenyewe, kuwa sehemu ya maisha yake na matokeo ya maisha yake, kuushiriki utii wake katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu kwa uhuru na uchungu” (Mng’ao wa ukweli au Veritatis Splendor n. 19). Kwa maneno mengine utendaji wake wa kimaisha unapaswa kuakisi historia nzima ya maisha ya Kristo hapa duniani, maisha ambayo yanahitimishwa na fumbo la msalaba; fumbo ambalo linaonesha utii wa hali juu hata katika hali ya uchungu. Hapa ndipo tunapoona maana ya mwaliko wa mtume Yakobo katika Waraka wake wa kudhihirisha imani yetu kwa matendo.
Mtume Yakobo anasema: “Imani isipokuwa na matendo, imekufa nafsini mwake.” Mwaliko huu wa ushuhuda wa kimaadili unatudai kuitambua hadhi tunayokuwa nayo baada ya kuunganika na Kristo. Fumbo la umwilisho limeuunganisha ubinadamu katika hali halisi na Mungu. Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu anafanya masakni ndani ya nafsi ya kila mmoja. Yesu Kristo ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli anatufunulia upya hadhi ya mwanadamu iliyotukuka na anatuonesha jinsi mwanadamu anavyopaswa kutenda akiwa ameungana na Mungu. Namna hiyo ya utendaji inajifunua katika fumbo la msalaba Mtakatifu ambalo sayansi yake inatuelekeza katika kuyaunganisha matendo yetu na Mungu. Kila tunachokifanya kiwe ni kwa ajili ya sifa na utukufu mkuu wa Mungu na kwa ajili ya wokovu wetu wanadamu. Hivyo mimi napaswa kuwa mkristo si kwa maneno tu bali niudhihirishe ukristo wangu kwa matendo yanayoakisi hadhi yangu ndani yangu.
Watu husema hivi: “nioneshe marafiki zako nami nitakueleza wewe u mtu wa namna gani.” Urafiki unawaunganisha watu wawili na kuwafanya washirikiane katika shida na raha. Rafiki huingia katika uwanja wa maisha ya mwenzake na kuyafanya kuwa yake. Ndivyo tunavyopaswa na sisi kuwa mbele ya Yesu Kristo ambaye anatuita pia rafiki zake. Yeye anatuita rafiki zake kwa sababu ametushirikisha utu wake ambao umeufunua na kuusimika uwepo wa Mungu kati yetu: “lakini Ninyi nimewaita rafiki; ka kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu” (Yn 15:15). Leo hii Yesu Kristo anataka tulikiri jina lake mbele ya mataifa kwa matendo yetu yanayounganika na Yeye. Yeye aliye rafiki yetu ametufunulia yote yaliyo moyoni mwa Baba yake na ametuonesha kwa mfano wa maisha yake yaliyofumbwa na fumbo la msalaba. Tumtamke kuwa ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai kwa ushuhuda wetu wa maisha ya msalaba.

SALA: Ee Yesu utupe ujasiri ya kuikiri imani yetu kwa matendo na pasipo woga wowote.