Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 14/09/2024

2024 SEPTEMBA 14: KUTUKUKA KWA MSALABA

Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama Sala ya Siku

SOMO 1. Hes 21:4-9

Siku zile jangwani, watu walimnung’unikia Mungu, na Musa, mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 78:1bc-2,34-38

1. Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu,
Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.
Na nifunue kinywa changu kwa mithali,
Niyatamke mafumbo ya kale.

(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.

2. Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta;
Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.
Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao,
Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wako. (K)

3. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao,
Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.
Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake,
Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. (K)

4. Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema,
Husamehe uovu wala haangamizi.
Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake,
Wala haiwashi hasira yake yote. (K)  

SOMO 2. Fil 2:6-11

Yesu Kristo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

INJILI. Yn 3:13-17

Yesu alimwambia Nikodemo: Hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.

 TAFAKARI

MSALABA NI USHINDI: Tunapiga magoti mbele ya Msalaba ili kuutazama, kuuabudu na kujifunza mambo ya kiroho. Ninapoutazama Msalaba ninaona sura inayovutia: Sura ya upendo. Na upendo una sifa zifuatazo: “Huvumilia; hufadhili; hahusudu; hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hauoni uchungu; haufurahii udhalimu; hufurahi pamoja na ukweli; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote…”(rej. 1Kor 13:4-7). Tunapoadhimisha kutukuka kwa Msalaba tunaadhimisha kutukuka kwa upendo, huruma, msamaha na uvumilivu wa Mungu. Ninapoungalia Msalaba ninaona fahari yangu; fahari ya mfuasi wa Kristu. Ni fahari ya kujivunia kama asemavyo Mt. Paulo Mtume, *”Mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo… ” (Gal 6:14). Ninapouangalia Msalaba ninamwona Yesu akinialika kumfuta.”Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate”(Mt 16:24). Msalaba ni nguvu yetu; Msalaba ni matumaini yetu kwani “Paalipo na Msalaba kuna wokovu.”

SALA: Ee Yesu utupe nguvu ili tuuchukue Msalaba wetu pasipo kuchoka.