Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/09/2024

2024 SEPTEMBA 13: IJUMAA-JUMA LA 23 LA MWAKA

Mt. Yohane Krisostomi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 3

SOMO 1. 1 Kor 9:16-19, 22b-27

Ijapokuwa naihubiri injili, sina la kujisifia, maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilionao katika injili. Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya injili ili kuishiriki pamoja na wengine. Je! Hamjui ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 84: 3-6, 12

1. Nafsi yangu imezionea kiu nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai.

(K) “Maskani zako zapendeza kama nini,
Ee Bwana wa majeshi. “

2. Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)

3. Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. (K)

4. Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao,
Bwana atatoa neema na utukufu.
Hatawanyima kitu chema
Hao waendao kwa ukamilifu. (K)

INJILI. Lk 6:39-42

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, “Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi.

TAFAKARI 

TUJICHUNGUZE SISI KWANZA: Injili ya leo ina mambo ya busara sana, lakini yaliyo dhahiri: kipofu hawezi kuwaongoza kipofu wengine; hatuwezi kuthubutu kurekebisha kasoro za watu wengine wakati sisi wenyewe tumejaa mambo ya kusahihishwa. Ikiwa tunataka kubadilisha watu wengine basi lazima tuanze na sisi wenyewe; ikiwa tunataka kuinjilisha wengine basi lazima kwanza tujiinjilishe weneywe. Tunafanya haya ili tusishutumiwe kwa unafiki, tukionyesha tusivyo. Tunasaidia wengine, tunawafundisha na kuwaongoza sio kwa sababu tuko katika nafasi ya kuwasaidia, kuwaongoza au kuwafundisha na sisi ni bora kuliko wao bali kwa sababu tunayafanya kwanza, sisi wenyewe. Na kwa hivyo ikiwa tunataka kuwa viongozi na waalimu kwa wengine, basi lazima tuwe na maono wazi ya mahali tunapoenda na ramani inayoonyesha njia. Ikiwa hatima yetu ni mbinguni, basi kuna njia moja tu na njia hiyo ni njia ya msalaba wa Yesu Kristo. Ni lazima tujitahidi kuwa kama Yeye, Kristo; lazima tujifunze kutoka kwake. 

SALA: Ee Yesu utupe neema ya kuwa mfano bora kwa wenzetu.