Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/09/2024

2024 SEPTEMBA 11: JUMATANO-JUMA LA 23 LA MWAKA

Mt. Felix
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 3

SOMO 1. 1 Kor 7:25-31

Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu. Basi, naona hili kuwa jema, kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo. Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke. Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili; nami nataka kuwazuilia hayo.  Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu. Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 45:11-12, 14-17

1. Sikia, binti, utazame, utege sikio lako,
Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.
Naye mfalme atautamani uzuri wako,
Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.

(K) Sikia, binti, utazame, utege sikio lako.

2. Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu,
Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.
Atapekekwa kwa mfalme
Wanawali wenzake wanaomfuata. (K)

3. Watapelekwa kwa furaha na shangwe,
Na kuingia katika nyumba ya mfalme.
Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako,
Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote. (K)

INJILI. Lk 6:20-26

Yesu aliinua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahieni siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni; maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.

TAFAKARI

UJASIRI KUSIMAMIA TUNU ZA KIINJILI: Kristo katika hotuba yake ya nyikani anawapa matumaini maskini, waliokandamizwa, wanaolia sasa na wanaoteseka kwa ajili ya kulishuhudia jina na kazi zake. Kwa mfano kuwa maskini hakuwezi kuchukuliwa ni heri au baraka katika jamii, lakini Kristo analiona hilo kwa namna tofauti. Matumaini ya maisha baada ya kifo yanawatuliza maskini kwani wanatambua wataurithi uzima wa milele. Kuwa tayari kuteseka kwa ajili ya Injili ya Kristo sio jambo jepesi na la kuzoea katika hali ya kawaida. Kusimama imara kwa ajili ya ukweli, haki za kila mtu, amani na upatanisho kati ya watu wenye fikra na uelewa tofauti na tunu za kiinjili ni gharama kubwa sana. Kristo ni mfano kwetu kwani anatufundisha kuwa mtetezi wa wanyonge hata ikiwa ni kuutoa uhai, alikuwa tayari kudhihakiwa, kudharauliwa na hata kufa kifo pale msalabani kwani aliwapenda na kuwatetea walio kandamizwa. Tunahitaji kuwa majasiri vya kutosha kuendelea kumfuta na kushika mafundisho yake.

SALA: Ee Bwana Yesu utujalie kutamani zaidi ufalme wako kuliko mali na heshima za dunia hii.