Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/09/2024

2024 SEPTEMBA 10: JUMANNE-JUMA LA 23 LA MWAKA

Mt. Apollinari Franco
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 3

SOMO 1. 1 Kor 6:1-11

Je! Mtu wa kwenu akiwa ana dawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki wala si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa tutawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang’anywa mali zenu? Bali kinyume cha hayo ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang’anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu. Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 149:1b-6a, 9b

1. Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyika la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wako.

(K) Bwana awaridhia watu wake.

2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

3. Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
Aleluya. (K)            

INJILI. Lk 6:12-19

Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu.  Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.

TAFAKARI. 

TUITIKIE WITO WA KRISTO, TUSHIRIKI UTUME WAKE: Bwana wetu Yesu Kristo alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha. Anatufundisha sisi kama wafuasi wake kudumu katika sala kama njia ya kuwasiliana na Mungu muumba wetu. Baada ya kusali, aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume. Kwa kuwachagua hawa mitume wake, amependa wawe karibu naye wajifunze kutoka kwake na baadaye awatume kuendeleza kazi yake ya kuhubiri na kuwapelekea watu habari njema ya wokovu. Amewachagua watu wenye uzoefu na umri tofauti tofauti akitufundisha kuwa Mungu hana ubaguzi. Aliposhuka kutoka mlimani, alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu wote walifika kumsikiliza na kuponywa magonjwa. Aliwaponya wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. Bwana wetu Yesu Kristo anawaalika watu wote kushiriki katika utume wa kuinjilisha na kuwawezesha wenzao kupata afya nzuri ya kimwili, kiakili na kiroho. 

SALA: Ee Bwana Yesu utujalie moyo wa sala kabla ya kufikia maamuzi ya utume wetu wa kila siku.