Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 05/06/2024

2024 JUNI 5 : JUMATANO-JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Bonifasi, Askofu na Shahidi
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma 4

Somo 1. 2 Tim 1:1-3, 6-12

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.

Wimbo wa Katikati. Zab 123:1-2

1. Nimekuinulia macho yangu,
Wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi
Kwa mkono wa bwana zao.

(K)Nimekuinulia macho yangu, ee Bwana.

2. Kama macho ya mjakazi
Kwa mkono wa bibi yake;
Hivyo macho yetu humlekea Bwana, Mungu wetu.
Hata atakapoturehemu. (K)

Injili. Mk 12:18-27

Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, walimwendea Yesu, wakamwuliza na kusema, “Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.  Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi katika hao?  Maana wote saba walikuwa naye.” Yesu akajibu, akawaambia, “Je, hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui Maandiko wala uweza wa Mungu?  Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai.  Hivyo mwapotea sana.”

TAFAKARI

KUNA MAISHA BAADA YA KIFO: Katekisimu yetu inatufundisha kuwa Mungu alituumba ili tumjue tumpende tumtumikie na mwisho tuende kwake Mbinguni. Kwenda Mbinguni ni kuanza kuishi maisha ya umilele. Katika Injili ya leo Masadukayo wasioamini ufufuko wanajaribu kupinga ukweli huu. Katika kuwafundisha ukweli juu ya ufufuko na maisha ya baadaye Masadukayo wanafundishwa kuwa katika ufufuko tutakuwa na miili ya utukufu kama ya Malaika. Miili hii ya utukufu haihitaji kula kunywa kuvaa kuoa au kuolewa. Ni kuwa na muungano wa jumla na Mungu baada ya kifo. Kwa njia ya kifo tunazaliwa upya na kuanza kuishi maisha mapya. Masadukayo walifungwa na sheria zao za kale wakashindwa kufungua mioyo yao na kujifunza kwa Yesu. Tufungue mioyo yetu turuhusu mafundisho ya Yesu yalete mabadiliko katika maisha yetu. Sisi tunaoamini uwepo wa maisha baada ya kifo tuwaombee marehemu wetu hasa katika mwezi wa kumi na moja ili waweze kufufuka pamoja na Kristo na wawe waombezi wetu.

SALA: Ee Yesu unijalie imani katika maisha yajayo.