Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/05/2024

2024 MEI 11 : JUMAMOSI-JUMA LA SITA LA PASAKA

Mt. Fransisko wa Girolamo, Padre
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mdo 18:23-28

Paulo akiisha kukaa Antiokia siku kadha wa kadha aliondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Friagia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzaliwa wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohane tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe; naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Wimbo wa Katikati. Zab 47: 2-3, 8-10

1. Enyi watu wote pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana aliye juu mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.

(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.

2. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)

3. Wakuu wa watu wamekusanyika,
Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu.
Maana ngao za dunia zina Mungu,
Ametukuka sana. (K)  

Injili. Yn 16:23-28

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambayo sitasema nanyi tena kwa mithali; lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. Na siku ile mtaomba kwa jina langu; wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba.  Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.

TAFAKARI

MUUNGANO WETU NA MUNGU: Leo katika Injili Yesu anatuonesha umuhimu wa muungano wetu na Baba. Muungano wa namna hii unaruhusu au kuwezesha sala zetu kumwendea Baba kirahisi na kujibiwa maombi yetu. Tunapokuwa na muungano wa dhati na Baba na Mwana, sala yetu inakuwa kamili na furaha yetu inakamilika. Nje ya muungano huu sala yetu inakosa nguvu na furaha yetu siyo kamili. Tujiunge na Baba na Mwana hasa kwa maisha ya sala, kwa njia ya Neno la Mungu, kwa njia ya kupokea Sakramenti mbalimbali na kwa kufuata mafundisho ya mamlaka funzi ya Kanisa. Tutumie muda tulionao kuhuisha muungano wetu na Baba na Mwana kila wakati. Tunaposali daima tuwe katika muungano na Yesu na tusiwe peke yetu. Kamwe tusiwe na mashaka juu ya upendo wa Mungu kwetu. Lolote tunalomwomba kwa imani kupitia mwanae hakika tutafanikiwa. Mungu kamwe hawatupi wanae hata kama wanae watamkimbia yeye atawakimbilia.

Sala: Ee Mungu usiruhusu nijitenge nawe hata mara moja.