Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/09/2024

2024 SEPTEMBA 29: DOMINIKA YA  26 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma II

SOMO 1. Hes 11: 25-29

Bwana alishuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wapili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda Hemani; nao wakatabiri kambini. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee Bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii, na kama Bwana angewatia roho yake. 

WIMBO WA KATIKATI. Zab 19: 8, 10, 12-13, 14

1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana mi amini,
Humtia mjinga hekima.

(K) Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo 

2. Kicho cha Bwana ni kitakatifu
Kinadumu milele
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)

3. Tena mtumishi wako huonywa kwazo,
Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.
Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake?
Unitakase na mambo ya siri. (K)

4. Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi,
Yasinitawale mimi mimi.
Ndipo nitakapokuwa kamili,
Nami nitakuwa safi, bila kosa lililo kubwa. (K)

SOMO 2. Yak 5: 1- 6

Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.   

INJILI. Mk 9: 38-43, 45, 47-48

Yohane alimwambia Yesu, Mwalimu tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanamu, kwenye moto usiozimika. Na mguu wako ukikukosesha, ukate, ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe, ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humu funza wao hafi, wala moto hauzimiki.

TAFAKARI

WEMA WA MUNGU NI KWA AJILI YA BINADAMU WOTE
Mtume Paulo anatuambia: “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake” (Rum 12:4 – 5). Ni mahusia ya kitume yanayoimarisha ushirikiano wa kindugu katika jamii ya mwanadamu. Hapa tunaoneshwa utajiri wa vipawa tofauti ambavyo mwenyezi Mungu huwakirimia wanadamu kila mmoja kwa nafasi yake ili kusudi katika kushirikishana tuweze kuimarishana. Ukweli huu unasakafia usawa na haki katikati yetu. Upendo wa kimungu ndiyo msingi wa mahusiano haya ya kindugu.
Dominika hii tunakumbushwa juu ya wema huu wa Mungu ambao ananuia uwafaidishe watu wote. Tunaonywa kujiepusha na uchoyo, wivu na kujilimbikizia madaraka na mali kwa faida ya ufahari na mamlaka binafsi na badala yake kuwa tayari kushirikishana katika vipawa vyetu. Ukweli wa jamii inayokua kama wana wa Israeli wakati wa Musa ulihitaji ushirikiano wa watu wengine. Jamii yao iliendelea kutanuka na pengine kazi zilimwelemea Musa. Katika hekima yake kuu mwenyezi Mungu analing’amua jambo hilo na hivyo anawashirikisha wazee wengine. “Akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini.”
Wazee hawa walipewa wajibu wa kushughulikia matatizo madogomadogo ya Waisraeli na yale ya muhimu zaidi yalipelekwa kwa Musa. Hivyo tangu kale tunaanza kuona umuhimu wa kushirikishana madaraka, jambo ambalo linaanzia kwa Mungu na linapata baraka zake. Mwenyezi Mungu anaonesha wazi kuwa uwezo wake haufugiki kwa mtu mmoja tu bali anao uwezo wa kuutwaa uwezo kutoka kwa mtu mmoja na kuutawanywa kwa watu wengi na lengo lake ni kuleta ufanisi kwa watu wengi katika namna rahisi na ya haraka. Kanisa Katoliki katika nchi za Afrika Mashariki limetuonesha hilo kwa mfano kupitia njia ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ambazo zimewekwa kama vyombo vya uinjilishaji wa kina.
Lakini namna hii njema inazusha wivu na watu wanaanza kuchongeana. Ni kana kwamba wapo ambao hawakubaliani na mpango wa Mungu wa kuweka karama zake kwa watu wote. Hata Yoshua ambaye ndiye amekuwa mrithi wa Musa kwa ajili ya kuwaongoza Waisraeli kufika nchi ya ahadi, hata Mtume Yohane yeye ambaye anaelezewa kama mwanafunzi aliyependwa zaidi na Kristo hawakuwa salama katika hali hii ya wivu na husuda za kimadaraka na kutotaka wengine washiriki karama za Mungu. Yoshua anasema: “Ee Bwana wangu Musa, uwakataze.” Mtume Yohane kwa upande wake alishafanya maamuzi ya kumkataza: “tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.”
Inawezekana kuona kwamba hao wasio pamoja nasi ni kinyume chetu na kudhani kwamba tunaweza kumwekea Mungu mipaka katika utendaji wake. Lakini jibu la Kristo linaweka msingi: “asiye kinyume chetu, yu upande wetu.” Mtume Paulo anaonya mahali pengine juu ya tabia hiyo na kuonesha kuwa Roho Mtakatifu huvuma kadiri apendavyo: “Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu” (1Kor 12:3). Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vaticano wanafundisha kuwa ingawa Kanisa linajionesha katika jumuiya ya waamini ya kikatoliki lakini “alama nyingi za utakatifu na ukweli zinapatikana pia nje ya mfumo huu unaojulikana” (Mwanga wa Mataifa au Lumen Gentium, n.8)
Tujiulize leo tunawaangalia vipi wenzetu ambao wanaonekana kutoshirikiana nasi katika ibada au shughuli za Kanisa? Je, wale wa madhehebu mengine au dini nyingine kwetu wana nafasi gani kuelekea wokovu? Tunasahau kuangalia mambo mema wanayotenda watu hawa. Wanazingalia familia zao, wanaongoza vema jamii zao na kwa hakika wanapendwa na wenzao. Tukumbuke swali la mtoto mdogo hivi karibuni alilomuuliza Baba Mtakatifu Fransisko juu ya maisha ya baba yake baada ya kufa. Baba huyo alikuwa mpagani lakini kadiri ya mtoto yule aliipenda familia yake. Lililo la muhimu si kuwa mkristo tu na kutenda mema bali pia mema hayo hutendayo yaonekane kuenea, kukua na kuwagusa wengine na kwa upande wao kugeuka vyombo vya utendaji wa wema.
Leo tunaoneshwa kuwa upendo wa Mungu hauna mipaka. Upendo wake si maalum kwa ajili ya kundi fulani tu la watu bali ni kwa ajili ya wote. Ni wito wa kuwa na utayari wa kushirikishana mafanikio kwa wote. Kama wewe umepata leo furahi pamoja na wengine na kesho mwenzako akipata hata kama kinachofanana na wewe isiwe sababu ya wivu. Unapaswa kufurahi pamoja naye. Wema wa Mungu unakua na unapitia njia mbalimbali kwa ajili ya kuwafaidisha watu wote. Kinyume chake tunaingia katika kishawishi cha kupora mema ya Mungu na mbaya zaidi kujilimbikizia na kujikinai kuwa ni mali yetu wenyewe na tumeyapata kwa uwezo wetu wenyewe.
Mtume Yakobo anaonya juu ya tabia hii katika Waraka wake kwa watu wote. Yeye anasema: “Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo”. Mtume Yakobo hapingi utajiri bali anapinga wale wanaong’ang’aniana nao kiasi cha kuona maisha yao na maana ya uwepo wao ipo hapo tu. Watu hawa kwa sababu ya uchu wa mali na kutotaka wengine kuyafaidi mema ya Mungu wanadiriki hata kuwanyonya wale wanaowatumikia. Ni onyo kwa jamii ya wanadamu ambayo inaendelea kutumia nguvu zao kimadaraka, kiuchumi na kijamii kuendelea kuwakandaiza wengine wasiweze kushiriki katika wema wa Mungu. Namna hii inapoteza kabisa ladha ya kuuona utu wa jirani yake. Mmoja anaendelea kujifungia katika ubinafsi wake. Hiki ni kilema cha kiroho.
Kristo anahitimisha Injili ya leo kwa kutualika kila mmoja wetu kutafakari juu ya kilema chake ambacho kinamzuia kuwa Mwema na kuona umuhimu wa mwenzako katika kushirikishana mema ya Mungu. Tupate ujasiri wa kuving’oa vilema hivyo kama ni kikwazo kwa wengine kufikia uzima wa milele. Ingawa mkono ni muhimu na zawadi kutoka kwa Mungu usiogope kuung’oa na kuingia uzimani u kigutu kuliko kuwa na mikono miwili na “kwenda zako jehanam, kwenye moto usiozimika.” Ni afadhali kuacha kutekeleza karama uliyo kama ni katika hali ya wivu na husuda, katika hali ya kudharau na kutowajali wengine. Tekeleza karama uliyopewa bila uchoyo, wivu au husuda. Tambua kwamba mwenyezi Mungu anawashirikisha wote mema yake na katika hali hiyo tunakamilishana kila mmoja kwa nafasi yake.

SALA: Ee Bwana utupe ujasiri wa kuving’oa vilema vyetu vya kiroho ili tuweze kukutumikia wewe kiaminifu.