Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 28/09/2024

2024 SEPTEMBA 28: JUMAMOSI-JUMA LA 25 LA MWAKA

Mt. Wenseslao, Shahidi
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma I

SOMO 1. Mhu 11: 9 – 12: 8

Wewe, kijana uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako; lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia. Mkumbuke Muumba wako, siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, “Mimi sina furaha katika hiyo.” Kabla jua, na nuru, na mwezi, na nyota, havijatiwa giza; kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; na milango kufungwa katika njia kuu; sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; na binti za kuimba watapunguzwa; naam, wataogopa kilichoinuka; na vitisho vitakuwapo njiani; na mlozi utachanua maua; na panzi atakuwa ni mzigo mzito; na pilipili hoho itapasuka; maana mtu aiendea nyumba yake ya milele. Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; au kuvunjwa bakuli la dhahabu; au mtungi kuvunjika kisimani; au gurudumu kuvunjika birikani; nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!

WIMBO WA KATIKATI. Zab 90: 3-6, 12-14, 17

1. Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kasha la usiku.

(K) “Wewe Bwana, umekuwa makao yetu,
kizazi baada ya kizazi. “

2. Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameavyo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka. (K)

3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekia.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)

4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti. (K)

INJILI. Lk 9: 43-45

Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu.” Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.

TAFAKARI

TUTAFUTE UELEWA SAHIHI: Yesu anawajulisha wanafunzi wake juu ya Mateso yake. Alisema, “Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu (Lk 9:44).” Wanafunzi wake hawakuelewa alichomaanisha. Ingawa watu wengine hawakuelewa aina ya mapinduzi aliyokuwa akiyafanya Kristo, wanafunzi wake waliendelea kujenga mahusiano ya karibu naye. Walikuwa na imani naye, walishaweka matumaini yao kwake, wanampenda na wanaona kuwa anayafanya mambo yote vizuri. Alifanya kazi nzuri wakati wa ujana wake. Wanakuwa mashuhuda wa maneno na matendo yaliyothaminiwa sana na maskini, walionyanyaswa, waliokandamizwa, aliyofundisha kwa mamlaka na kusahihisha mifumo ya kimamlaka na kisheria iliyokuwapo. Hawakufikiri kwa matendo hayo mtu yeyote angemkasirikia. Pengine mambo ya msingi sana tunayopaswa kuyatafakari ni unabii wa Kristo ambao utatimizwa kwa sababu baadhi ya watu hawakumwelewa na hivyo wakafikiri anahatarisha nafasi zao au walikuwa na wivu au walimsaliti.  

SALA: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuelewa mafundisho yako, kustawi katika ukarimu na kuwa waaminifu kwako.