Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/09/2024

2024 SEPTEMBA 27: IJUMAA-JUMA LA 25 LA MWAKA

Mt. Vinsenti wa Paulo, Padre
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma I

SOMO 1. Mhu 3:1-11

Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; wakati wa vita, na wakati wa amani. Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo? Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 144: 1-4

1. Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu namwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia.

(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

2. Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue?
Na binadamu hata umwangalie?
Binadamu amefanana na ubatili,
Siku zake ni kama kivuli kipitacho. (K)

INJILI. Lk 9:18-22

Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, “Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani?” Wakamjibu wakisema, “Yohane Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmoja wapo wa manabii wa kale amefufuka.” Akawaambia, “Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani?” Petro akamjibu akasema, “Ndiwe Kristo wa Mungu.” Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo, akisema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.”

TAFAKARI. 

KRISTO NDIYE MASIHA ALIYETARAJIWA: Wayahudi walikuwa na mategemeo makubwa sana kwa masiha atakayekuja. Wengi wao walimsubiria masiha wa kisiasa na fahari za kidunia. Walisali ili ndoto yao itimie ya kumpata kiongozi wa kulipangilia taifa lao kuwa lenye mamlaka na fahari kubwa, atakayeifanya Israeli iwe katika nafasi ya kwanza kimataifa. Kristo Masiha aliyekuja alikuwa na mipangilio tofauti na hiyo, kwanza alilazimika kuchukua muda kusahihisha mtazamo wao wa mawazo. Aliwaelimisha watu juu ya mtazamo sahihi na asilia ya masiha, alivyoendelea kuwaelimisha alijidhihirisha kwao kama Masiha aliyeahidiwa. Kristo alikuja kuujenga Ufalme wa Mungu kwa kuzilea roho za watu katika maisha ya Kiroho. Alikuja sio kujenga mamlaka za kidunia na fahari za mali, bali alikuja avae taji la miiba na sio taji la dhahabu. Wewe unatarajia masiha wa namna gani? Mimi Kristo ndiye Masiha, Masiha anayetakasa, anayefundisha mema, anayewahudumia watu kwa upendo, anayeponya wagonjwa, anayewaweka huru waliofungwa na shetani.

SALA: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuyaelewa mafundisho yako na kuyaishi. Amina.