Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/09/2024

2024 SEPTEMBA 26: ALHAMISI-JUMA LA 25 LA MWAKA

Wat. Kosma na Damiano, Mashahidi
Rangi: Nyekundu

Zaburi: Juma I

SOMO 1. Mhu 1:2-11

Mhubiri asema, ubatili mtupu, “Ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake. Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, ‘Tazama, ni jambo jipya?” Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.”

WIMBO WA KATIKATI. Zab 90:3-6, 12-14, 17

1. Warudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kasha la usiku.

(K) “Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu,
kizazi baada ya kizazi. “

2. Wawagharikisha huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka. (K)

3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)

4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti. (K)

INJILI. Lk 9:7-9

Herode mfalme alisikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohane amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, “Yohane nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake?” Akataka kumwona.

TAFAKARI

KRISTO NI NANI KWANGU? Herode aliposikia habari za Yesu; kazi na mafundisho yake, watu walivyofikiri juu yake na kumwona wa muhimu na wa maana sana aliuliza huyu ni nani? Akatamani kumwona Yesu. Umaarufu wa Yesu ulifanananishwa na watu maarufu waliowahi kuishi kama Yohani Mbatizaji na Eliya. Herode kama mtawala alihangaishwa sana na umaarufu wa Yesu, ulimuweka njia panda, hakujua nini kitakacho fuata, pengine atapinduliwa. Ni ukweli ulio bayana kuwa Herode anakosa usingizi kwa sababu ya Yesu. Atakuwa aliona Utendaji wa Yesu umemvurugia mipango yake. Yesu alikuwa tayari kumpokea kama angekuwa tayari kufanya toba. Herode hakuwa tayari kushirikiana na neema ya Mungu, anaendelea kudumu katika ubatili na uovu wake. Ni wakati nasi tujitathmini, tunapata muda wa kutosha wa kujiuliza Kristo kwangu ni nani? Anayawezesha maisha yako kwa namna gani? Anahatarisha usalama wa maisha yako kwa namna gani? Au ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako? Katika Kristo mimi nina furaha, nina amani, nina utulivu, nina uzima wote. 

SALA: Ee Bwana uniwezeshe kuendelea kukutambua kuwa wewe ni Njia, Ukweli na Uzima nikupokee na kukuishi maisha yangu yote.