Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/09/2024

2024 SEPTEMBA 25: JUMATANO-JUMA LA 25 LA MWAKA

Mt. Nikolao
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma I

SOMO 1. Mit 30:5-9

Kila neno la Mungu limehakikishwa; yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo. Mambo haya mawili nimekuomba; usininyime matatu kabla sijafa. Uniondolee ubatili na uongo; usinipe umaskini wala utajiri; unilishe chakula kilicho kadiri yangu. Nisije nikashiba nikakukana, nikasema, “Bwana ni nani?” Wala nisiwe maskini sana nikaiba, na kulitaja bure jina la Mungu wangu.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 119:29, 72, 89,101, 104,163

1. Uniondolee njia ya uongo,
Unineemeshe kwa sheria yako.
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.

(K) “Neno lako ni taa ya miguu yangu. “

2. Ee Bwana, neno lako lasimama,
Imara mbinguni hata milele.
Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya,
Ili nilitii neno lako. (K)

3. Kwa mausia yako najipatia ufahamu,
Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
Nimeuchukia uongo, umenikirihi,
Sheria yako nimeipenda. (K)         

INJILI. Lk 9:1-6

Yesu aliwaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. Akawaambia, “Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. Na nyumba yo yote mtakayoingia kaeni humo, tokeni humo. Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao.” Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri Injili, na kupoza watu kila mahali.

TAFAKARI.

KUINJILISHA, TUJALI MAHITAJI YA KIROHO NA KIMWILI: Wakati fulani Rais Wilson waliwahi kusema; “Hakuna anayempenda jirani yake akiwa na tumbo wazi.” Alilolisema ni la muhimu sana kwani mwanadamu ni mwili na roho. Kushughulika na roho bila kuujali mwili huko ni kuukataa ukweli kuwa vyote viwili ni muhimu na vinategemeana. Hatuwezi tukawazungumzia watu mambo ya kiroho ya mbinguni na hatufanyi lolote au hatuzungumzii ya ulimwenguni na mahitaji yao ya kimwili. Yote mawili yanaenda pamoja kwani mwanadamu ni mwili na roho. Tukifuatilia maombi ya Mithali anatambua hili la msingi pia kuwa mwili na roho vinaenda pamoja anamwomba Bwana asimfanye maskini wala tajiri, kama maskini asije akaiba au kama tajiri asije akashiba akamkana. Kristo amewaelekeza mtume wake wahubiri na kuponya. Kristo anapowatuma mitume anawaelekeza kuwahudumia watu kwa mahitaji ya kiroho na ya kimwili. Nasi pia katika utendaji wetu tujibidishe kujiendeleza na kuwaendeleza wengine kiroho na kimwili kwa kujielimisha na kuelimisha wengine pia. 

SALA: Ee Bwana, neema yako ituwezeshe kuyahudumia ipasavyo na kwa wema mahitaji ya watu wako ya kiroho na kimwili. Amina.