Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 15/10/2024

2024 OKTOBA 15: JUMANNE: JUMA LA 28 LA MWAKA

MMt. Teresia wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma IV

SOMO 1. Gal 5:1-6

Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 119:41, 43-45, 47-48

1. Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi,
Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
Nami nitamjibu neno anilaumuye,
Kwa maana nalitumainia neno lako.

(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi.

2. Nami nitalitii milele na milele.
Naam, milele na milele.
Nami nitakwenda panapo nafasi,
Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. (K)

3. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,
Ambayo nimeyapenda.
Na mikono nitayoyapenda,
Nami nitazitafakari amri zako. (K)

INJILI. Lk 11:37-41

Yesu alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, “Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.

TAFAKARI

KINYAGO: “Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu.” Katika vinyago vingi ambavyo vimetumika katika kuficha maumivu na hisia za kuumizwa, dini ni mojawapo. Katika dini watu wameweza kuonesha sura nzurri na safi kwa nje, na kuficha yale yaliyo ndani ya mtu yaani maumivu mateso na hata maovu (uozo). Hapa Yesu anawaalaika watu wale ambao wanvaa vinyago kuficha hali zao mbaya za dhambi kuachana kabisa na hali hiyo. Waepuke kujifanya wema machoni pa watu. Mwaliko huo huo tunapatiwa sisi pia. Tunapaswa kuwa tayari kukubali kwamba tumejaa uovu ndani yetu, na hivi tumwombe Mungu aanze kutujenga kutoka ndani kuja nje. Vinyago tunavyojivika havitufaidii chochote. Maisha yetu halisi, yaani vile Mungu alivyotuumba ndiyo sura hiyo tunayopaswa kuonesha mbele ya watu. Jambo hilo linahitaji unyenyekevu wa hali ya juu kabisa.

SALA: Ee Mungu utujalie neema ya kuchunguza undani wetu ili matendo yetu yaakisi kilicho ndani.