Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/10/2024

2024 OKTOBA 13: DOMINIKA YA 28 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma IV

SOMO 1. Hek 7:7-11

Naliomba, nikapewa ufahamu; nalimwita Mungu, nikajiliwa na roho ya Hekima. Naliichagua kuliko fimbo za enzi na viti vya enzi, wala mali sikudhani kuwa ni kitu ikilinganishwa nayo; wala sikuifananisha na kitu cha thamani; mradi dhahabu yote ya nchi ni kama mchanga kidogo mbele yake, na fedha itahesabiwa kama udongo. Naliipenda kupita afya njema na uzuri wa sura, hata zaidi ya nuru nikataka kuwa nayo, kwa maana mwangaza wake haufifii kamwe. Na pamoja nayo nikajiliwa na mema yote jamii, na mikononi mwake mali isiyoweza kuhesabika.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 90:12-17

1. Utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee, Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako.

(K) ” Utushibishe kwa fadhili zako ili tufurahi. “

2. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi, tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa,
Kama miaka ile tuliyoona mabaya. (K)

3. Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako,
Na adhama yako kwa watoto wao.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Naam, kazi ya mikono yako uithibitishe. (K)

SOMO 2. Ebr 4:12-13

Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.

INJILI. Mk 10:17-30

Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza.  Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?  Yesu akamwambia, kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja, Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.  Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni Rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.  Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu. Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto na mashamba pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

TAFAKARI

UTAJIRI WA KWELI NA WA KUDUMU HUKAMILISHWA KATIKA HEKIMA YA MUNGU
Wanadamu wote tunayo shauku ya mafanikio katika maisha yetu. Kila mmoja hujitahidi kwa namna mbalimbali kutafuta fanaka katika maisha. Mfanyakazi hufanya kazi kwa bidii ili kupata kipato zaidi; mfanyabiashara hutafuta mbinu mbalimbali ili kuongeza biashara yake na mwisho kipato kiongezeke; mkulima hali kadhalika hufanya kilimo chake kwa ustadi na bidii kubwa kusudi apate mazao mengi na hatimaye kipato chake kiongezeke. Hakika namna hii huendana na amri ya Mungu kwa mwanadamu tangu uumbaji: “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha” (Mwa 1:28). Hivyo kuwa na utajiri wa mali au kuwa na madaraka au kuwa na umaarufu kwa sababu ya vipaji vyako si jambo baya. Ni karama tunazopokea kutoka kwa Mungu kwa ajili ya kuendelea kuratibisha kazi ya uumbaji.
Kutoka katika agizo hilo la Mungu mwanadamu anapaswa kuona muunganiko wa kazi ya mikono yake na uwepo wa Mungu. Hivyo mafanikio yote anayoyapata yanapaswa kuunganishwa na hekima yake kuu. Mungu ndiye sababu ya uwepo wa vitu vyote na katika Yeye ndipo tunachota hekima. Neno la Mungu katika Dominika hii linatukumbusha juu ya utajiri huo wa hekima ya Mungu. Somo la kwanza linaanza kwa kutuagiza kuwa, ili kuwa na hekima tunapaswa kuomba kutoka kwa Mungu kwa sababu Yeye ndiye asili ya hekima yote. “Kila hekima hutoka kwa Mungu na katika Yeye hukaa milele” (YbS 1:1). Hekima hiyo ni mwanga au nuru ya kutuongoza ili kuweza kuutumia vema ulimwengu huu. “Yeye ameivumbua njia yote ya hekima akampa Yakobo mtumishi wake na Israeli mpendwa wake” (Bar 3:37).
Hakuna kiumbe chochote, hata wafalme, ambacho kinachoweza kujipatia hekima hii. (rej. Bar 3:15-31) Hivyo jambo la kwanza tunalodaiwa ni ukaribu wetu na Mungu kwa njia ya imani. Mfalme Solomoni ni kielelezo kwetu. Yeye aliomba akisema: “nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya.” (rej. 1Fal 3:6 – 9). Hiyo ndiyo inapaswa kuwa hamu ya mwanadamu. Utajiri wa namna yoyote, uzuri wote, afya njema si kitu kama mmoja anaikosa hekima ya Mungu. Hii ni kwa sababu mwangaza wake kamwe hautui. Kila mmoja wetu katika maisha anaitwa kutathimini kilicho cha thamani. Je, ni kujilimbikizia tu utajiri na madaraka bila kuwa na hekima? Hekima hiyo anavyosema mwandishi wa somo wa kwanza ni nuru na ni ya kudumu. Ni nuru ya kutuongoza vema ili kufikia ufanisi wa kweli.
Mali na mafanikio ya ulimwengu huu kamwe yasituondolee imani yetu kwa Mwenyezi Mungu, matokeo yake ni kuingia katika kujitafutia mali na kufanya matumizi ya mali katika namna zisizofaa. Madhulumu, uchoyo, unyonyaji na ubadhirifu wa mali na zaidi uharibifu wa hadhi ya mwanadamu kwa ajili ya mali au karama au madaraka ya Dunia hii huchagizwa na umbali wa mwanadamu na Mungu. Falsafa za kumpatia mwanadamu uhuru bandia, uhuru ambao umeyatoa mamlaka ya Mungu juu ya kazi yote ya uumbaji zimesababisha mwanadamu kupoteza sifa aliyopewa tangu uumbaji ya kuuratibu ulimwengu huu. Tunaalikwa kujitathimini na kugutuka kuwa uhuru wetu wanadamu unapata thamani na unakuwa wenye tija pale tu unapoangaziwa na hekima kutoka juu.
Hamu ya kijana wa simulizi la Injili inatuingiza katika utajiri wa hekima ya Mungu. Kijana huyu anapiga mbio kumkimbilia Kristo. Kitendo hiki kinaonesha kujiamini kwa mwanadamu katika uwezo wake. Tabia ambazo zinajioesha zaidi katika vijana wetu leo. Umri wa ujana hupambwa na hali ya kujiamini kupita kiasi na kuona kuwa yote yanawezekana katika uwezo wa mtu husika. Ndiyo maana tunaona kijana huyu anajisifia mbele ya Kristo. Kwamba anazifahamu hizo amri na amezishika ni nini sasa kitamzuia kuurithi ufalme wa mbinguni? Ni kana kwamba anajipambanua kuwa yeye binafsi yu mkamilifu. Ameweza yote kwa kuwa anao uwezo. Lakini mwisho wa yote tunaambiwa kuwa Yule kijana “alikunja uso … akaenda zake kwa huzuni.” Hii inatusukuma kutafakari kile kilochosababisha mwisho huo mchungu na wa huzuni. Pamoja na kuwa na nguvu kama kijana, pamoja na kuwa na mali nyingi, pamoja na kudhani kwamba ameshika vema amri za Mungu aliishia kuingia katika huzuni.
Huzuni hiyo ilisababishwa na takwa la Kristo la kuutumia utajiri wake na kuwashirikisha wengine. Kristo alimfunulia jinsi hekima ya Mungu inavyoelekeza katika ukamilifu. Kwa maneno mengine alimwalika kijana huyo kujifunza katika maisha ya Kristo namna ya kuwa mwema. Kristo katika kenosi yake alionesha namna hiyo ya mwanadamu kuwa Mwema mbele ya Mungu. Wema huo huturandanisha maisha yetu na Mungu na hivyo kumfanya Mungu aendelee kububujika kutoka katika maisha yetu. Kijana huyu alipomuita Kristo “Mwalimu Mwema” bila shaka alikwishamwona na hivyo kutaka kujifananisha naye katika wema huo. Hekima ya Mungu ambayo inajifunua katika Kristo na ambayo hutupeleka katika wema hututaka kuuratibisha ulimwengu huu kadiri atakavyo Mungu. Hii ni ile hali ya kunuia kuyafanya yote kuona na kuonja upendo wa Mungu. Hivyo tunapoelekezwa kuendana na hekima hiyo tunapaswa kuona furaha.
Kwa maneno mengine, wema Mungu huonekana katika ufanisi wa wanadamu wote. Jukumu la mwanadamu la kuratibisha ulimwengu linapaswa limsukume na kuwa na utayari wa kushirikiana na wote ili kufikia mafanikio ya kweli. Yeye ambaye anapewa karama ya aina moja na Mungu anaalikwa kuutumia utajiri huo ili kumfaidisha na mwingine na hivyo mwisho wa siku kazi yote ya uumbaji kuwa katika hali ya ufanisi. Hii ndiyo kazi ya kuuratibisha uumbaji. Hapa tunaona maana ya Amri mpya ya upendo aliyotuachia Kristo, kwamba upendo wetu kwa Mungu unaendelea kusambaa kwa yeye aliye pembeni yangu na tunaweza kuongeza kwamba husambaa kwa vyote vinavyonizunguka. Mungu hausiani na mtu mmoja mmoja katika utengano na wengine bali katika muunganiko.
Somo la pili linatuonesha kuwa Kristo ni Neno la Mungu aliyemwilika. Yeye ndiye ufunuo wa hekima ya Mungu kwetu. Kwa kufanyika mwanadamu kamili Kristo anaonja na kufahamu sawasawa kile kilichopo ndani ya wanadamu. Hatuwezi kujificha mbele la Mungu kwani neno lake linapenya hadi ndani ya nafsi zetu na kuyafahamu yote. Kristo kama Neno na Hekima hiyo ya Mungu anatusindikiza katika kina cha nafsi zetu ili kuweza kulitambua neno lake na kujazwa hekima yake. Hivyo tuombe neema ya Mungu ili kuwa na uwezo na ujasiri wa kuungana naye katika neno lake na zaidi katika Sakramenti zake hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii itatuimarisha katika hekima ya Mungu na hivyo kuunganisha shughuli zetu zote katika kuelekea ukamilifu wa kweli upatikanao kwa Mungu. Hapo kwa hakika tutajirandanisha na wema Kristo ambao unaufunua na kuusimika wema wa Mungu katikati yetu.

SALA: Ee Yesu utusaidie tufungamane nawe zaidi kuliko mali za dunia.