Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 17/10/2024

2024 OKTOBA 17: ALHAMISI: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Ignasi wa Antiokia, Askofu na Shahidi
Rangi: Nyekundu

Zaburi: Juma IV

SOMO 1. Efe 1: 1-10

Paulo mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu wanaomwamini Kristo Yesu. Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa Baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 98: 1-6

1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu,
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

(K) Bwana ameufunua wokovu wake.

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)

INJILI. Lk 11:47-54

Yesu aliwaambia wanasheria: “Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara.  Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.” Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.

TAFAKARI

TUJIIFUNZE KUWASAIDIA WENGINE: Tunaposoma Biblia na maelezo yake, tunaposikiliza redio, tunapotafuta elimu, tunapotumia muda wetu wa mapumziko katika kumbi kubwa tukijadili mambo yahusuyo Mungu, ni vyema tuweze pia kuwashirikisha wengine. Pamoja na kuwa na sifa kubwa wataalamu wa Biblia katika aya tulizosikia wanaonekana kushindwa kabisa. Kadiri tunavyotafuta maarifa, tunapaswa kutafuta na njia za kuwashirikisha wengine, ili waweze kuyatumia, na yawasaidie kuwa karibu zaidi na Mungu. Yesu anawakosoa Mafarisayo na wanasheria kwa sababu wanaosha nje yao wakati ndani ni kuchafu. Wanakumbuka hata kulipa zaka ya mazao katika bustani zao lakini wanapuuzia haki. Wanawafungia watu mizigo mizito ya mahitaji ya kidini. Hawakubali ukweli kuhusu Yesu, na kuwazuia wengine wasiupokee ukweli. Wanakosea kwa kuangalia mambo ya nje na kupuuzia mambo ya ndani kabisa mioyoni mwao. Hata leo sisi pia tunafanya hivyo hivyo pale tunapowasaidia watu tukiwa na lengo la kuonekana na sio kusaidia kwa upendo. Tusiwe wakristo wa kuonekana kwa nje tu. 

SALA: Bwana Yesu tunakuomba utujalie maneno na matendo yetu yaakisiwe na maisha yetu katika Kristo.