Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 16/10/2024

2024 OKTOBA 16: JUMATANO: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Hedwiga, Mtawa/Mt. Margarita Alakok, Bikira
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma IV

SOMO 1. Gal 5:18-25

Mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 1: 1-4, 6

1. Heri mtu Yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

(K) “Wanaokufuata, Ee Bwana,
watakuwa na nuru ya uzima. “

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)  

INJILI. Lk 11:42-46

Yesu aliwaambia Mafarisayo: “Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.” Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, “Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wanasheria, Ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

TAFAKARI

WATAALAMU: Ikiwa umeweza kukariri aya zote za Biblia katika maktaba yako au ya parokia yako au ya chuo chako, kama maisha yako hayaakisi imani katika Mungu mmoja na Bwana wetu Yesu Kisto, hilo halikufaidii kitu. Ikiwa umeweza kupitia nukuu zote katika Biblia na huku umeshindwa kuwashirikisha wale walio masikini Habari njema, kukariri kwako hakukufaidii kitu. Ikiwa unaweza kuyataja majina yote ya Mungu kutoka Agano la Kale hadi Agano jipya, na hujawahi kuwaambia jirani zako hata mara moja habari za Yesu Kristo, wewe utakuwa ni nani basi? Je! ni mtaalamu wa Maandiko Matakatifu? Ikiwa kwa kufanya hivyo unakuwa au unaitwa mtaalamu wa Maandiko Matakatifu, hilo lina faida gani kwako? “Ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.” Kile tunachoamini, tunachosema na tunachofanya kinapaswa kuakisi imani yetu. Tofauti na hayo tutakua upatu uvumao na elimu yetu na vyote tufanyavyo havitakuwa na faida yoyote kwetu.

SALA: Bwana Yesu, Neno lako na liakisiwe katika maisha yetu, tuweze kuwavuta wengine kwako.