Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/07/2024

2024 JULAI 27: JUMAMOSI-JUMA  LA 16 LA MWAKA

Wat. Aurelio na Natalia, Wafiadini
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Tazama Sala ya Siku

Soma 1. Yer 7:1-11

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana.Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa. Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya. Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; kama hamwonei mgeni wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe; ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele. Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia. Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukuzia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua; kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote? Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.

Wimbo wa Katikati. Zab 84:3-6, 8, 11

1. Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
Naam na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu,
Vinamlilia Mungu aliye hai.

(K) “Maskani zako zapendeza kama nini,
ee Bwana wa majeshi.”

2. Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake.
Kwenye madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)

3. Heri wakaao nyumbani mwako
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. (K)

4. Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa awabu
Nyumbani mwa Mungu wangu,
Kuliko kukaa hema za uovu. (K)

Injili. Mt 13:24-30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi.  Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

TAFAKARI

MUNGU ANATUPATIA MUDA WA KUBADILI MIENENDO YETU: Katika sehemu ya somo la Injili ya leo mfano tunaopewa wa ngano na magugu unamhusu kila mmoja wetu. Tunapoishi tunaishi kama ngano au gugu? Baada ya maisha ya hapa duniani kila mmoja atajihukumu kulingana na jinsi alivyoishi hapa duniani. Tukiifuata vizuri njia ya Kristo, wakati wa mavuno tutakusanywa katika kundi lake la Ufalme wa Mbinguni. Mtu akishawishika na shetani akipanda uovu katika maisha yake atafananishwa na gugu ambalo halimfurahishi Mungu na siku ya mavuno hutengwa na ngano safi. Ila Mungu ni mwingi wa huruma na Upendo amemwekea mwanadamu muda wa kutosha kujitathimi na kufanya mabadiliko katika maisha yake. Katika somo la kwanza nabii Yeremia amelitaja hilo vizuri anaposema “Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.” Ndivyo Kristo anavyomfundisha mwanadamu mwenye utashi kwamba akiweza kujitathmini na kutubu atapokea huruma ya Mungu. 

Sala: Ee Bwana Neema yako ituwezeshe kutambua tunapokosea na kufanya toba.