Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 24/07/2024

2024 JULAI 24: JUMATANO-JUMA  LA 16 LA MWAKA

Mt. Sharbel Makhluf
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma 4

Somo 1. Yer 1: 1, 4-10

Maneno ya Yeremia, mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani waliokuwa katika Anathothi, katika nchi ya Benyamini. Neno la Bwana lilinijia, kusema, kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.” Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto;’maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao; maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe. Asema Bwana.Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, “Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.”

Wimbo wa Katikati. Zab 71: 1-6, 15, 17

1. Nimekukimbilia wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe.

(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.

2. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda siku zote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)

3. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu wewe daima. (K)

4. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)

Injili. Mt 13:1-9

Yesu alitoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema,” Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga. Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie.”

TAFAKARI.

TUSHIRIKIANE NA MPANGO WA MUNGU: Uelewa wa tangu zamani ni kuwa, Mungu anamtuma kila mtu ulimwenguni akiwa na ujumbe maalum, akiwa na wimbo maalumu wa kuwaimbia wengine, na akiwa na tendo maalumu la upendo la kufikisha kwa jamii. Hakuna yeyote atakaeupeleka ujumbe wangu alionipa Mungu kwa watu ila mimi mwenyewe. Hakuna yeyote aliye mdogo au mdhaifu, au mzee sana kwamba hawezi kuufikisha ujumbe huo kwa wengine. Kila mmoja wetu atambue, kuna utume wakutimiza hapa duniani. Nabii Yeremia alivyotumwa na Mungu hakuyaelewa haya anajitetea kuwa yeye ni mtoto tu. Mungu anamwambia usiseme kuwa wewe ni mtoto, maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao; maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe. Ndivyo pia kila mwanadamu anayepaswa kusimamia, kutenda na kupeleka wema kwa wengine anapaswa kutiwa moyo kwa maneno hayo. Usijifikirie upo mwenyewe au unafanya kwa nguvu zako mwenyewe bali Mungu ndiye anayetuwezesha. 

Sala: Ee Bwana tuwezeshe kuutambua mpango wako na kushirikiana nawe. Amina.