JUMANNE: JUMA IV LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA IV
Mt. Gilbert, Padre
Kuzaliwa: Alizaliwa Sempringhan(Uingereza)
Utume: Alisoma Ufaransa (Paris). Baada ya kurudi alianzisha shule ya watoto na watu maskini na kufundisha jinsi ya kupata utakatifu. Aligawa mali alizorithi kwa maskini. Alianzisha monasteri mbili ya masista wa Wabenediktini na wanaume wa Wagilberti.
Kufariki : Mwaka 1190.
SOMO 1. Ebr. 12:1-4
Kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito. Na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambayo kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustaimilisha msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwaga damu, mkishindana na dhambi.
WIMBO WA KATIKATI. Zab. 22:25-27, 29-31-32
- Nitaziondoa nadhiri zangu mbele zao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele.
(K) Wanaokutafuta, Ee Bwana, watakusifu.
- Miisho yote ya dunia itakumbuka,
Na watu watamrejea Bwana,
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,
Humwinamia wote washukao mavumbini. (K) - Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyeyafanya. (K)
INJILI. Mk. 5:21-43
Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga-songa. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro na Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.
TAFAKARI
IMANI HAIJALISHI TAJIRI AU MASKINI: Wapo wanaobeza mambo ya imani na kusema eti wanaotakiwa kuwa watu wa sala ni maskini kwa vigezo kuwa hawana shughuli nyingi na pili eti ili Mungu awahurumie. Usishangae ukakutana na mtu mwenye uwezo akisema, ‘nikasali kwani nimekosa nini!’ Huyu mkuu wa sinagogi kwa wakati ule ni mtu mkubwa, lakini pamoja na ukuu huo bado ananyenyekea na kuona kuwa Yesu ni wa msaada kwake. Kuna baadhi yetu tukijaliwa uwezo au cheo hatushikiki, hatuambiliki. Tunajikweza, unakuwa na dharau hata kwa kanisa. Wahenga walisema “maskini akipata matako hulia mbwata” wakimaanisha kuwa na majivuno na dharau. Leo Mgerasi anatuasa kuwa pamoja na kufanikiwa bado nafasi ya Mungu iko pale pale, tusiipuuzie, tuone kuwa yeye ndiye mpaji wa vyote.
Sala: Tunakuomba Bwana hata pale tunapojaliwa baraka mbalimbali katika maisha yetu bado tuwe wanyenyekevu.